Dida afunguka ishu yake na Manula Simba - 2

Friday July 12 2019

 

By Olipa Assa

KATIKA sehemu ya kwanza makala haya na kipa aliyemaliza mkataba wake Simba, Deogratius Munishi ‘Dida’, alifunguka alivyouza mama ntilie akimsaidia mama yake kabla ya kusajiliwa na Manyema FC na baadaye kuchezea Simba, Yanga, Azam. Endelea…

ALIKOTOKEA DIDA

Anasimulia kwamba alikuwa muokota mipira (Ball Boy) kwenye Uwanja wa Uhuru mwaka 2000 na kwamba ikitokea Simba inafanya mazoezi alikuwa anaenda kumuomba kocha ili kufanya nao ambapo anawataja kina Mohamed Mwameja na Kelvin Mhagama ndiyo waliomvutia.

Baadaye, Dida anasema, walianzisha timu yao ya mtaani kwa vijana wote aliokuwa anaokota nao mipira, waliita Ball Boys, ambayo mechi za mitaani walizokuwa wakicheza zilifichua zaidi kipaji chake.

Anasema alijitambua kwamba ni kipa baada ya kucheza gombania goli, mchezo ambao anayefunga ndiye anasimama langoni na anadai alipokuwa akisimama golini alikuwa hodari wa kuzuia mpaka mechi inaisha, jambo analosema lilizidi kumwaminisha kwamba yeye ni mlinda mlango.

“Tulikuwa tukicheza mechi za mtaani, walikuwa wananipanga niwe kipa na nilikuwa sifungwi, hapo ndipo nilipotambua nafasi yangu kwamba natakiwa niwe kipa, niliendelea kuwa hivyo mpaka leo hii ambapo najulikana ndani na nje ya nchi,” anasema.

Advertisement

MANYEMA YAMPA MKE

Dida anasema alisajiliwa na Manyema FC iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza na akaipandisha kucheza Ligi Kuu msimu wa 2007-08. Baada ya kucheza nusu msimu tu kwenye Ligi Kuu, kiwango chake kikawavutia Simba, wakamsajili fasta mwaka huo huo.

Lakini kabla ya kujiunga na Simba anasema Wanamsimbazi hao walicheza dhidi ya Manyema kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, mechi anayodai ilijaza watu ambapo ilipatikana pesa nyingi na yeye alipewa Sh 15,000 ambayo ndio ilikuwa pesa yake kubwa ya kwanza ya jasho lake kuishika mkononi kwa wakati huo.

“Ndio pesa kubwa niliyoishika kwa kipindi chote nilichocheza Manyema tangu tukiwa Daraja la Kwanza hadi Ligi Kuu. Matumizi yake yalikuwa kununua vocha kwa kuwa kipindi hicho nilikuwa sina majukumu.

“Lakini pia sitaisahau Manyema kwani ndio iliyonikutanisha na mke wangu. Wakati tumeweka kambi mkoani Songea, alikuja kuangalia mechi, nilimuona ni msichana mstaarabu, mpole na anayejielewa, tukapendana na ndiye mke wangu mpaka leo,” anasema.

Anasema alianza kuishi naye mwanamke huyo aliyezaa naye watoto wawili na Juni mwaka jana ndiyo wakaibariki ndoa yao.

KASEJA AMKIMBIZA MSIMBAZI

Dida anasema alipojiunga na Simba, kikosini wakakutana ‘meza moja’ makipa watatu wenye ubora wa juu pamoja na Ally Mustapha ‘Barthez’ na Juma Kaseja.

Hata hivyo, yeye na Barthez walikuwa katika wakati mgumu kupata namba kwani kwa wakati huo Kaseja alikuwa ndiye kipa namba moja wa Simba na nahodha wa Taifa Stars.

“Nilikaa benchi sana, Kaseja kipindi hicho alikuwa kwenye kiwango cha juu, alikuwa anatuambia mimi na Barthez tukaze la sivyo tutaondoka bila kuonja mechi hata moja.

“Kaseja alikuwa anadaka mwenyewe hadi mechi zile za kirafiki, kuna wakati mwingine alikuwa anaumwa, lakini alikuwa anajikaza na kudaka mwenyewe, ile ilinifunza kwamba soka ni mapambano na sio lele mama.

“Baadaye nikaachana na Simba na kwenda kucheza Oman kwenye klabu ya Al-Tihad 2010 na 2011 nikarejea nyumbani na kujiunga na Mtibwa Sugar ambako nilicheza msimu mmoja,” anasema.

AZAM, YEYE NA MANULA

Dida alijiunga na Azam FC mwaka 2012 akitokea Mtibwa Sugar, wakati huo Aishi Manula alikuwa kikosi B, anasema ndiye alikuwa kipa namba moja.

Anasimulia alivyoishi na Manula namna alivyokuwa anamfuata na kumwambia anatamani awe kama yeye, anakiri akilini mwake yalikuwa yanamjia maneno aliyokuwa akiambiwa na Kaseja kwamba wasipokaza wataishia kukaa benchi.

“Sikuchukia maneno ya Kaseja, nilimwambia mdogo wangu Manula, kwamba pambana unaweza ukafanya makubwa kuliko mimi, niliishi naye kwa upendo sana, nilifanya naye mazoezi kwenye timu ya wakubwa, alikuwa na juhudi sana.

“Maisha ni mzunguko ningeishi vibaya na Manula nikiwa Azam FC, unadhani ingekuwaje wakati nimemkuta Simba akiwa kipa namba moja, hili liwe fundisho kwa wachezaji kutoishi kwa unafiki, tushindane kwa kazi bora na sio roho mbaya.

“Nakumbuka nilipojiunga na Yanga, mwaka 2013 mpaka 2017 Kaseja alinikuta akitokea Simba, hakupata shida kuishi na mimi kwa sababu alikuwa mkongwe na anaelewa kwamba bila juhudi kazi sio rahisi,” anasema.

KIWANGO CHA MANULA

Amekizungumzia kiwango cha Aishi Manula kwamba kinatokana na nidhamu yake ya mazoezi na kujitambua anataka kuwa nani.

“Manula ni kipa mwenye uwezo ndio maana anategemewa kwenye kikosi cha Taifa Stars na tegemeo Simba, kikubwa aendelee kupambana aone huo ni mwanzo safari bado inaendelea,” anasema.

Ameenda mbali na kumtaja Beno Kakolanya kwamba ana uwezo wa juu hivyo anaamini ataonyesha ushindani wa kweli wa kumfanya Manula asijibweteke.

“Mazoezi ambayo nilikuwa nafanya yalikuwa yanamfanya Manula ajitume kwa bidii akijua wazi nikipata nafasi atasugua benchi, kuna wakati hata kama kocha hayupo nilikuwa namuongoza mimi,” anasema.

SIMBA, YANGA ALIVUNA MATAJI SIO PESA

Dida anafichua kwamba hakuwahi kuvuta pesa ndefu nyakati za nyuma akiwa Simba na Yanga.

Anakiri kwamba msimu wa 2018/19 ndio mara ya kwanza kwake kuonja mkwanja mrefu, Simba ilipomtoa Afrika Kusini kwenye timu ya Pretoria University.

“Nilicheza Simba awali 2007- 10, nikajiunga Yanga 2013-17 sikuwahi kupata pesa kubwa zaidi ya kutengeneza jina na kuchukua mataji,” anasema.

Usikose sehemu inayofuata kesho Jumamosi uone kitu kisichotarajiwa alichomfanya Yusuf Manji, na jinsi biashara ya dawa za kulevya ilivyoathiri familia yao.

Advertisement