Diamond amfuata Waziri Mwakyembe kushabikia Aston Villa ya Samatta

Muktasari:

Samatta anakuwa mchezaji wa tatu kutoka Afrika Mashariki kucheza Ligi Kuu ya England baada ya Victor Wanyama wa Kenya na Saido Berahino wa Burundi.

Dar es Salaam.Mwanamuziki Diamond Platnumz amefuata nyayo za Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe kuwa rasmi mashabiki wa klabu ya Aston Villa baada ya Mbwana Samatta kusajiliwa na timu hiyo ya Ligi Kuu England.

Katika posti yake aliyoweka muda huu katika ukurasa wake wa Instagram, Diamond aliandika: "Nlichokifanya ni kuhama kwenye team yangu na Kuhamia @avfcofficial , na akihama tena team nyingine nahama nae.....najua pengine una team uipendayo ila ombi langu ukishindwa kuhamia kama Mie,  walau iwe team yako ya pili ili tuzidi kumpa Nguvu @samagoal77  CHAMP!!!.....🌍🏆🌍 #HiiNiTanzaniaMpya"

Ujumbe wa Diamond kutangaza kujiunga kushabikia timu hiyo ulikuja baada ya Waziri Mwakyembe kutangaza kuwa shabiki rasmi wa Villa katika ujumbe aliouandika mapema:

"Hongera Mbwana kwa hatua hii kubwa uliyofikia katika soka. Pamoja na kuiletea nchi yako sifa duniani, umewapa matumaini makubwa watoto na vijana (wa kike na kiume) wanaopenda soka nchini, kufika hapo ulipofika. Kwani wanajua kuwa umefika hapo si kwa kubahatisha, bali kwa juhudi binafsi, kujituma bila kutetereka wala kuchoka na kwa nidhamu ya hali ya juu unayoionesha daima ndani na nje ya uwanja.

"Nina imani utafanya makubwa Aston Villa. Kaa ukijua kuwa hauko peke yako huko ughaibuni, uko na Watanzania wote kwa maombi/dua katika kukutakia mafanikio mema. Leo natangaza kwamba nahamia rasmi Aston Villa FC. Baba hamwachi mwana peke yake!"

Haraka baada ya Samatta kuandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kusajiliwa katika Ligi Kuu ya England, watu mbalimbali maarufu nchini wakiwamo viongozi wa kiserikali waliandika meseji za kupongeza hatua hiyo.

Kuchelewa kwa Diamond kutoa pongezi zake kulikosolewa na wengi katika mitandao ya kijamii wakimtuhumu kumuonea wivu staa hiyo huku wengine wakiweka picha ya Samatta na Diamond na kuwapambanisha nani mwenye pesa nyingi.

Samatta, 26, amesaini mkataba wa miaka minne na nusu wa kuitumikia klabu hiyo inayotumia Uwanja wa Villa Park na anakuwa mchezaji wa tatu kutoka Afrika Mashariki kucheza kwenye Ligi Kuu ya England baada ya Victor Wanyama wa Kenya na Saido Berahino wa Burundi.