Diamond: Wanawake waambieni wanaume wenu watumie Kondomu

Wednesday July 10 2019

 

By Rhobi Chacha

Dar es Salaam. Mwanamuziki, Naseeb Abdul 'Diamond Platnumz' amesema,  wanawake wawe na sauti ya kuwakomalia wanaume kutojamiana bila kutumia Kondomu.
Hayo ameyasema, leo Jumatano Julai 10, 2019 kwenye mkutano wa wasanii wa lebo ya  Wasafi na Tume ya kudhibiti Ukimwi (TACAIDS).
Diamond amesema, kutokana na Tume ya kudhibiti Ukimwi (TACAIDS)  kuwadhamini  katika tamasha la Wasafi Festival litakaloanza  Julai 19,2019 atahakikisha anatoa elimu kwa wanawake watakaohudhuria.
Kuhusu TACAIDS kushirikiana nao kwenye tamasha hilo, Diamond amesema wamekuja wakati mzuri kwani lengo si kutoa burudani tu, bali na elimu kwa vijana kuhusu maisha yao.
Kwa upande wake, Jumanne Issango ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa TACAIDS, amesema mkakati wa nne wa kudhibiti Ukimwi, vijana ndio wamepewa kipaumbele.
"Takwimu zilizotolewa hivi karibuni zinanyesha vijana kati ya umri wa miaka 15 hadi 24 wanachangia maambukizi mapya ya Ukimwi kati ya watu 70,000 kwa mwaka, huku asilimia 80 wakiwa wasichana. Hivyo mikakati yetu ni kuona elimu inaenda zaidi kwa vijana kwani hawa ndio nguvu kazi ya Taifa,"amesema Issango.
Kwa upande wa Ofisa Sanaa wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Bonnah Masenga, amesema TACAIDS hawajakosea kwani wasanii ni watu wanaosikilizwa na kuangaliwa na watu ikiwemo kwenye kurasa zao kwenye mitandao ya kijamii.

Advertisement