Dante atibua mambo, Ajibu atuliza

Muktasari:

  • Yanga itashuka leo ikiwa ni mchezo wao wa tatu tangu ipate viongozi wapya chini ya Mwenyekiti wao, Dk Mshindo Msolla na Makamu wake, Fredrick Mwakalebela waliochaguliwa Jumapili iliyopita kwenye Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo.

MZUKA umepanda huko Jangwani, baada ya nahodha wao Ibrahim Ajibu kurejea tena uwanjani, huku beki wa kati wa timu hiyo akitibua mambo.

Yanga iliyopoteza mchezo wao wa tano msimu huu kwa kunyukwa bao 1-0 na Biashara United, leo Jumanne inatarajiwa kuvaana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Uhuru, huku ikimkosa Dante, lakini jambo la furaha ni kurejea kwa Ajibu aliyekosa mechi iliyopita kutokana na kuugua ghafla.

Yanga jana ilifanya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya mchezo huo kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam, huku Ajibu akiwa mmoja ya wachezaji wanaotarajiwa kuweko kikosini.

Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh alisema kabla ya mechi ya leo walipanga kufanya mazoezi siku mbili kwa maana ya juzi Jumapili na jana Jumatatu lakini sababu zilikuwa nje ya uwezo wao zilisababisha kufanya hivyo na kupata siku moja tu ya kufanya mazoezi.

Saleh alisema Ajibu amerejea kikosini baada ya kupona malaria aliyougua ghafla wakijiandaa kutoka Iringa walikoenda kucheza na kufungwa na Lipuli katika nusu fainali ya Kombe la FA ili kwenda Musoma kuvaana na Biashara waliowacharaza katika Ligi.

Mratibu huyo alisema kwa sasa limebaki jukumu la Kocha Zahera kuamua kumtumia Ajibu ama la katika mchezo huo ambao Ruvu watataka kulipa kisasi cha kufungwa mabao 3-2 katika pambano lao la kwanza na wababe hao wa Jangwani.

“Tulishindwa kufanya mazoezi jana (juzi) kutokana na shida ya usafari ambayo tulikutana nayo Mwanza, kwani tulitakiwa kuondoka saa 1:00 usiku Ijumaa, lakini ilishindikana tukaambiwa ndege imechelewa kufika tusubiri mpaka saa 4:00 usiku, tulikaa mpaka muda huo,” alisema.

“Cha kushangaza imefika saa 4, usiku tunaambiwa ndege imepata hitilafu kwa maana hiyo tusubiri tena, tukajikuta tunaondoka pale Mwanza saa 8, usiku na kufika Dar es Salaam, saa 10 alfajiri Jumamosi tukiwa tumechoka,” alisema Saleh.

Yanga itashuka leo ikiwa ni mchezo wao wa tatu tangu ipate viongozi wapya chini ya Mwenyekiti wao, Dk Mshindo Msolla na Makamu wake, Fredrick Mwakalebela waliochaguliwa Jumapili iliyopita kwenye Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo.

Mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania wanahitaji ushindi leo mbele ya Ruvu ili kuendelea kufukuzana na watani zao Simba ambao jana jioni walikuwa wakimalizana na Azam FC katika mechi yao ya marudiano.

Hata hivyo, watakuwa na kazi kubwa kwani, Kocha wa Ruvu AbdulMutik Haji ‘Kiduu’ amesisitiza hatakubali kupoteza tena mchezo wao na Yanga, kwani bado hawapo katika nafasi nzuri kulingana na uwiano wa tofauti za alama walionazo wao na timu nyingine.