Dante aigomea Simba kweupee

Muktasari:

  • Beki huyo alisema takwimu zinaonyesha Simba inasumbuliwa na timu ndogo na wakianza kutoka mikoani zaidi mambo yatawabadilikia.

YANGA jana Jumatano ilikuwa Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza kuvaana na Mbao FC, ikiwa na kumbukumbu mbaya ya uwanja huo, lakini huku nyuma beki wake wa kati aliyewahi kujifunga mbele ya Wauza Mbao hao, Andrew Vincent ‘Dante’ ametangaza kuigomea Simba.

Dante alijifunga kwenye pambano la nusu fainali ya Kombe la FA mwaka 2017 na kuitemea timu yake taji iliyokuwa inalishikilia kwa msimu huo, lakini juzi akizungumza na Mwanaspoti alisema licha ya kufungwa na Simba katika mechi ya watani, lakini haoni Msimbazi wakitetea taji.

Beki huyo alisema ameuangalia msimamo wa Ligi Kuu na mechi zilizobaki na kutamka kuwa hata kama Simba wamewafunga lakini bado ni mapema kusema timu hiyo itatetea taji na badala yake kutaka mashabiki wasubiri hadi mwisho wa msimu wataona mambo yatakavyokuwa.

Dante alisema wao kama wachezaji wameyasahau matokeo ya kufungwa na Simba, sasa wanaangalia mechi zijazo za ligi kwa kuwa ligi bado.

Dante alisema kufungwa na Simba haina maana kwamba ushindi wao utawapa ubingwa na kwamba ligi bado ngumu lolote linaweza kutokea.

“Simba haiwezi kuwa bingwa kirahisi hivyo ligi bado, na mambo magumu zaidi yanakuja nadhani tusubiri ndipo mtaamini maneno yangu,” alisema Dante.

Beki huyo alisema takwimu zinaonyesha Simba inasumbuliwa na timu ndogo na wakianza kutoka mikoani zaidi mambo yatawabadilikia.

“Simba ilipoteza na Mbao hakuna aliyedhani hilo litatokea, Yanga tutaendelea kuifukuza Simba mpaka kieleweke bado tunaamini tutawavua ubingwa msimu huu,” alisema.

Alisema wamekubaliana ushindi katika mechi zijazo ni kitu kisichokwepeka. Kabla ya mechi ya jana Yanga ilikuwa na alama 58 baada ya mechi 24 huku Simba ikiwa nafasi ya tatu na pointi zao 42 kutokana na mechi 17.