Dadi za kibabe Man United v Man City chapa ilale

Muktasari:

Rekodi zinaonyesha kwamba kumeshapigwa Manchester Derby 177 huku United wakishinda 73 na City wameshinda mechi 51, sare ni 52.

London, England. KIPUTE cha mahasimu ndio kimewadia mwanangu, ndio ni Manchester Dabi ambako safari hii shoo ya kibabe inapigwa pale Etihad. Baada ya zote kupata ushindi kwenye mechi zao za Ligi ya Mabingwa Ulaya, sasa shughuli inarudi katika Ligi Kuu ya England.
Kesho Jumapili, Jose Mourinho ataliongoza jeshi lake kumfuata hasimu wake mkubwa Pep Guardiola kwenye dimba la Etihad kuwania kusaka kama sio pointi tatu basi hata moja, lakini mpinzani wake huyo hatakubali kuona hilo likitokea.
Pep anataka kuendeleza rekodi ya ushindi dhidi ya Mourinho ambaye amekuwa akikutana na wakati mgumu kila wanapokutana tangu wakiwa La Liga.
Hata hivyo, rekodi zinaonyesha kwamba kumeshapigwa Manchester Derby 177 huku United wakishinda 73 na City wameshinda mechi 51, sare ni 52, lakini mechi nyingi zikiwa kwenye utawala wa Sir Alex Ferguson.
Kwa sasa Guardiola na jeshi ambalo ndio mabingwa watetezi wa EPL, wanaongoza ligi na pointi zao 29. Hawajapoteza mechi hata moja huku Mourinho akiwa nafasi ya nane na pointi 20.
Nani atacheka kati ya Guardiola na Mourinho, lakini Mwanaspoti halitaki uumize kichwa kabisa na hapa linakupa mechi tano kali za Manchester Derby zilizotikisa EPL.

5. Man United 1-1 Man City (Aprili 21, 2001)
Unaposoma matokeo hayo hapo juu, utashangaa imekuwaje mechi ya sare ya 1-1, ikaorodheshwa kati ya mechi tano kali za Manchester Derby. Mechi hii inakumbukwa kutokana na tukio lililomtokea, kiungo wa zamani wa Man City, Alf Inge Haaland.
Sio jina maarufu sana, lakini kwa hakika shabiki ‘damu’ wa timu hizi atakuwa anamfahamu. Ni katika derby hii, iliyopigwa Aprili 21, 2001, ndipo jina la Haaland lilipopata umaarufu.
Rafu mbaya aliyochezewa na kiungo wa zamani wa Man United, Roy Keane ndio iliyoupa mchezo huu umaarufu. Ni rafu mbaya iliyohitimisha ndoto za beki huyu.
Paul Dickov, alitoa pasi ya kizembe kuelekea langoni na kumlazimisha kipa wa City, Carlo Nash, kufanya maamuzi magumu ya kumkwatua Ole Gunnar Solksjaer. Mwamuzi akaizawadia United penalti. Teddy Sheringham, akauweka mpira kambani. United wakaongoza 1-0.
Hata hivyo, katika dakika ya 84, wakati wengi wakiamini United wamepata ushindi muhimu Old Trafford, Steve Havey akafanya yake. Mwisho wa siku, matokeo yakasomeka 1-1.

4. Man United 4-2 Man City (Aprili 12, 2015)
Kabla ya mtanange huu, United walikuwa hawajapata ushindi katika Derby nne zilizotangulia. Kwa kifupi waliingia Old Trafford wakifahamu fika kuwa wao ni kibonde. Hivyo ndivyo walivyoamini. Wengi waliamini hivyo pia.
Lakini, kama kuna mtu ambaye aliamini tofauti siku hiyo, alikuwa ni Ashley Young. Ilikuwa ni zaidi ya imani ya kishujaa.
Bao moja na asisti mbili zilitosha kufuta hisia zilizojengeka katika mawazo ya wengi kabla ya mechi hii.
City ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya nane, kupitia kwa Sergio Aguero, aliyepokea pasi murua kutoka kwa David Silva. Dakika sita baadaye, Ashley akasawazisha.
Muda mfupi baadaye akammegea Marouane Fellaini pasi safi iliyozaa bao la pili. Kabla bao hilo halijapoa, Juan Mata akaenda kumsalimia Joe Hart. Ubao ukasomeka 3-1, kabla Chris Smalling hajaongeza la nne, mpishi akiwa ni Ashley.
Zikiwa zimesalia dakika chache mpira umalizike, Aguero akatupia la pili, akiunganisha krosi ya Pablo Zabaletta. Matokeo yakasomeka 4-2.
Huo ukawa ukawa mwisho wa dharau za Manchester City. Mwendelezo wa kiburi cha Mashetani Wekundu.
3. Man City 4 - 1 Man United (Septemba 22, 2013)
Sir Alex Ferguson alipoondoka Man United, watu walitabiri ungekuwa mwisho wa ubabe na mwanzo wa maisha magumu ya mashetani wekundu kwenye ulimwengu wa soka.
Kibarua cha kwanza cha David Moyes, kikawa ni Manchester Derby. Septemba 22, mwaka 2013, vijana wa Moyes walisafiri hadi Etihad. Kilichotokea kikathibitisha utabiri wa hali ngumu inayowakabili United. Walipigwa 4-1 na vijana wa Manuel Pellegrini.
Wauaji katika mchezo huo, uliotawaliwa na City, wakiwa ni Sergio Aguero (aliyetupia mawili), Yaya Toure na Samir Nasri. Bao la United lilifungwa na Wayne Rooney. Huu ukawa mchezo wa pili, ulioshuhudia Mashetani wekundu wakibatizwa kwa moto.

2. Man United 4-3 Man City (Septemba 20, 2009)
Wakati mashabiki wa timu hizi walipojazana pale Old Trafford, kusubiri mtanange huu, hawakuwa na habari, kungekuwa na idadi kubwa ya mabao. Hawakujua mabao yangefika saba. Ila ilikuwa hivyo. Katika dakika ya pili ya mchezo, Wayne Rooney alishacheka na wavu. Gareth Barry akasawazisha muda mfupi baadaye na kulazimisha mechi kwenda mapumziko ikiwa sare ya 1-1.
Dakika ya 49 Darren Fletcher akawarudisha United uongozini kabla Craig Bellamy hajasawazisha dakika tatu baadaye.
Fletcher akaiongezea United la tatu, zikiwa zimesalia dakika chache tu mechi kumalizika, lakini dakika ya 90 Bellamy akasawazisha.
Wakiwa wanaamini mechi inaisha kwa sare ya 3-3, Mwamuzi Martin Atkinson ndio kwanza alikuwa anawaza kuongeza dakika sita za nyongeza.
Dakika ya 94, Michael Owen akapiga la nne na kufanya ubao usomeke 4-3. Hadi kipyenga cha Atkinson kinapulizwa kuashiria mwisho wa dakika 96 za kutoka jasho uwanjani Old Trafford, ni Man United ndio waliotoka dimbani wakicheka.

1. Man United 1-6 Man City (Oktoba, 2011)
Sio timu zote zimeweza kuwa na kiburi cha kupata ushindi wa 6-1 dhidi ya wapinzani wao wa jadi, katika mechi ngumu ya Derby. Hata hivyo, Man City walifanya hivyo, Oktoba 2011, tena wakiwa ugenini. Hii ilikuwa zaidi ya dharau.
Kibaya zaidi, matokeo hayo yalikuwa ni ‘zawadi’ ya mapema ya bethidei kwa Rooney, ambaye alikuwa anatimiza miaka 26 siku iliyofuata.
Mario Balotelli, alipiga la kwanza na la pili (dk 12 na 60), Sergio Aguero akapiga la tatu (dk 69).
Darren Fletcher akafunga la kwanza kwa Man United, kabla City kushindilia mabao matatu ndani ya dakika nne. Wamaliziaji wakiwa ni David Silva na Edin Dzeko aliyetupia mara mbili.