Croatia yameguka, beki akosa nusu fainali leo

Wednesday July 11 2018

 

Moscow, Russia. Beki wa Croatia, Sime Vrsaljko atakosa mchezo wa leo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya England kutokana na majeraha.

Mchezaji huyo anayecheza nafasi ya beki wa kulia, aliumia goti katika mchezo walioshinda mabao 4-3 kwa penalti dhidi ya Russia.

Nyota huyo wa Atletico Madrid alilazimika kutoka dakika ya saba baada ya kuanza mchezo katika dakika za nyongeza kutokana na jeraha hilo.

Beki wa zamani wa Tottenham Hotspurs, Vedran Corluka anatarajiwa kuchukua nafasi ya mchezaji huyo katika mchezo huo uliopangwa kuchezwa Uwanja wa Luzhniki.

Corluka ambaye ni beki mkongwe mwenye miaka 31, anatarajiwa kucheza nafasi ya beki wa kati na Dejan Lovren.

“Tumeishuhudia England katika mechi zote, tunajiamini ingawa tuna wachezaji chipukizi. Hatuna presha,” alisema Corluka.

Alisema ingawa Croatia haikuwahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia, lakini haina maana kwamba hawana nafasi ya kufanya vyema katika fanali hizo.

Croatia imecheza dakika 120 katika mechi mbili tofauti na kushinda kwa penalti ikiifunga Denmark katika hatua ya makundi kabla ya kuinyuka Russia katika mechi ya robo fainali.

Advertisement