Coutinho ataka maelezo Barca

Monday January 14 2019

 

BARCELONA, HISPANIA .KIUNGO wa Kibrazili, Philippe Coutinho anataka maelezo kutoka kwenye Bodi ya Wakurugenzi wa Barcelona kutokana na namna anavyofanyiwa na kocha wa timu hiyo, Ernesto Valverde.

Ripoti ya Cadena Cope inadai, Coutinho anataka kufahamu sababu zinazomfanya Kocha Valverde asimtumie kwenye mechi za timu hiyo na kumweka benchi.

Kwa sasa kwenye kikosi cha Barcelona, Coutinho amekuwa akijikuta akiwekwa benchi huko Ousmane Dembele akipewa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza jambo ambalo linamvuruga Mbrazili huyo kwa sasa.

Coutinho licha ya kufunga kwenye mechi ya kipigo kutoka kwa Levante kwenye Copa del Rey, staa huyo wa zamani wa Liverpool alikosolewa na Kocha Valverde kuhusu uchezaji wake.

“Wakati nilipokuwa simchezeshi Dembele kila mtu alikuwa akiniliuliza,” alisema Valverde.

“Sasa anacheza na Coutinho hachezi, mambo yaleyale na maswali yaleyale yamekuwa yakiulizwa tena. Wachezaji ni lazima wafanye kazi ili kupata nafasi.

“Hana furaha, anapaswa kupambana, lakini katika njia moja au nyingine Coutinho anapaswa kutupatia kilicho bora.”

Siku za karibuni, Coutinho amekuwa akiripotiwa kuwekwa kwenye orodha ya wachezaji wa kupigwa bei na Barcelona huku Man United ikihusishwa na mpango wa kunasa.

Advertisement