Coutinho, wengine tisa out Barcelona

Muktasari:

Kiungo wa kimataifa wa Croatia, Ivan Rakitic ambaye amekuwa akihusishwa na Manchester United naye ni miongoni mwa mastaa wanaoweza kupisha njia huku tayari Barcelona ikiwa imemnasa kiungo wa kimataifa wa Uholanzi, Frenkie de Jong kutoka Ajax.

BARCELONA, HISPANIA. REAL Madrid inatamba sokoni. Imenunua mastaa watano na bado ipo sokoni. Inataka kurudisha heshima. Lakini upande wa pili kule kwa wapinzani wao Barcelona wao wanataka kutembeza fagio kwanza kabla ya kuingia sokoni.

Mastaa 10 wa Barcelona wanatazamiwa kuondoka katika dirisha hili la uhamisho wakiongozwa na nyota wa kimataifa wa Brazil, Philippe Coutinho ambaye mpira umemkataa tangu alipotua kwa dau la Pauni 145 milioni kutoka Liverpool Januari mwaka jana.

Klabu mbalimbali zikiongozwa na PSG zinadaiwa kumtaka staa huyo wa zamani wa Liverpool katika dirisha hili huku Barcelona ikitarajiwa kupata hasara kwa kumuuza pungufu ya Pauni 90 milioni ili aweze kuondoka.

Kipa wa akiba wa Barcelona, Jasper Cillessen ambaye ni kipa wa kimataifa wa Uholanzi pia anatazamiwa kuondoka klabuni hapo baada ya kushindwa kumng’oa kipa namba moja, Marc-Andre ter Stegen na tayari amehusishwa na uhamisho wa Pauni 25 milioni kwenda Porto ingawa dau lake linatajwa kuwa Pauni 26 milioni.

Kiungo wa kimataifa wa Croatia, Ivan Rakitic ambaye amekuwa akihusishwa na Manchester United naye ni miongoni mwa mastaa wanaoweza kupisha njia huku tayari Barcelona ikiwa imemnasa kiungo wa kimataifa wa Uholanzi, Frenkie de Jong kutoka Ajax.

Beki wa kulia, Nelson Semedo ameomba kuuzwa wakati huu Kocha Ernesto Valverde akimtumia zaidi Sergi Roberto na tayari Atletico Madrid imeonyesha nia ya kumchukua staa huyo wa kimataifa wa Ureno.

Mwingine ambaye yupo mbioni kuondoka ni winga wa Kibrazili, Malcom ambaye wakala wake ameanza mazungumzo na mabosi wa Barcelona kuangalia uwezekano wa kuondoka Nou Camp msimu mmoja tu baada ya kuwasili klabuni hapo.

Malcom aliwasili akitokea Bordeaux ya Ufaransa kwa dau la Pauni 37 milioni huku Barca ikiifanyia umafia Klabu ya AS Roma ambayo ilikuwa imejiandaa kumtwaa staa huyo lakini dakika za mwisho akaibukia Nou Camp. Hata hivyo, ameshindwa kupata nafasi ya kudumu kikosini hapo na anafikiria kuondoka.

Kiungo wa pembeni, Denis Suarez ambaye alicheza kwa mkopo bila ya mafanikio Arsenal naye anatazamiwa kuondoka jumla katika dirisha hili huku akisakwa na klabu za Italia wakati staa mwingine, Rafinha naye hayumo katika mipango ya kocha.

Kiungo wa kimataifa wa Ureno, Andre Gomes anatazamiwa kuuzwa jumla Everton baada ya kung’ara katika kipindi chake cha mkopo kwa klabu hiyo ya Merseyside na mazungumzo baina ya pande hizo mbili yanakwenda sawa ingawa Gomes pia anatakiwa na Tottenham na West Ham.

Makinda Marc Cucurella na Sergi Palencia wanaweza kuuzwa jumla klabuni hapo huku kiungo mkongwe, Kevin-Prince Boateng pamoja na Jeison Murillo, ambao walichukuliwa kwa mikopo kutoka katika klabu za Sassuolo na Valencia wakitazamiwa kurudishwa katika klabu zao.

Kinda, Jean-Clair Todibo, aliyenunuliwa katika dirisha la Januari akitokea Toulouse ya Ufaransa anaweza kuuzwa kwenda kwingineko ingawa Barcelona itaweka kipengele cha kumnunua kwa bei chee katika siku za usoni.

Baada ya kufanya ufagio kwa mastaa hao mbalimbali, Barcelona inatazamiwa kuingia sokoni kwa nguvu baada ya kutishwa na nguvu ya usajili ambayo imefanywa na watani zao, Real Madrid ambao tayari wamenunua mastaa watano katika dirisha hili.

Mastaa walionunuliwa na Madrid ni pamoja na nyota wa kimataifa wa Ubelgiji, Eden Hazard kutoka Chelsea, Luka Jovic kutoka Frankfurt, Rodriyo kutoka Santos ya Brazil, Eder Militao kutoka Porto na Ferland Mendy kutoka Lyon ya Ufaransa.