Coastal Union waipania Yanga Uwanja wa Mkapa

Wednesday September 30 2020

 

By OLIVER ALBERT

KOCHA wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya JKT Tanzania juzi utachochea morali katika kikosi chake wanapokwenda kuikabili Yanga Jumamosi usiku.

Kabla ya mchezo wa juzi dhidi ya JKT Tanzania, Coastal Union ilikuwa moja ya timu tatu ambazo hazikuwahi kushinda tangu Ligi Kuu Bara ianze msimu huu wala kufunga bao lolote.

Licha ya kwamba ilipata ushindi baada ya beki wa kati wa JKT Tanzania, Edson Katanga kujifunga akiwa katika harakati za kuokoa, Mgunda amesema muhimu pointi tatu.

Mgunda alisema walikuwa katika presha kubwa ya kutafuta matokeo kabla ya mchezo huo lakini wanashukuru wamepata ushindi ambao umerejesha matumaini katika kikosi chake.

“Tulikuwa katika wakati mgumu kwani tu lianza ligi vibaya baada ya kucheza michezo mitatu na kupoteza miwili na kutoka sare mmoja hivyo hali hiyo ilikuwa ikituumiza na tuliweka malengo kuhakikisha mechi ya JKT Tanzania lazima tupambane tushinde.

“Ugeni wa wachezaji wengi katika kikosi chetu unachangia kuanza ligi kwa kusuasua kwani ukiangalia wachezaji wangu wengi wa kikosi cha kwanza wa msimu uliopita wameondoa na kusajiliwa na timu nyingine hivyo ni kama tunaanza upya lakini naamini muda si mrefu tutarudi katika ubora wetu kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Advertisement

“Bado tuna mapungufu katika baadhi ya maeneo hasa katika umaliziaji kuna tatizo bado ambalo inabidi tulifanyie kazi kabla ya mchezo ujao dhidi ya Yanga ili kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema.

Advertisement