City Bulls yatema ubingwa wa RBA rasmi

Bingwa mtetezi wa Ligi ya Mpira wa Kikapu mkoa wa Dar es Salaam (RBA), Vijana City Bulls (VBC) imevuliwa rasmi ubingwa huo.

VBC imeshindwa kutetea taji hilo baada ya kuruhusu kipigo cha pointi 80-75 dhidi ya timu ya jeshi ya ABC katika mechi ya tatu 'game three' jana Jumapili usiku kwenye uwanja wa Bandari, Kurasini.

Timu hiyo ilianza vizuri mechi ya kwanza ya robo fainali (play-off) kwa kuichapa ABC pointi 81-71, lakini ikaambulia kipigo kama hicho kwenye mechi ya marudiano, matokeo ambayo yalisababisha zicheze mechi ya tatu na ya kuamua timu itakayofuzu kucheza nusu fainali kuungana na JKT, Kurasini Heat na Oilers.

Kocha wa ABC, Haleluya Kavalambi alisema matokeo waliyopata kwenye mechi ya tatu yalitokana na nidhamu ya mchezo waliyoionyesha.

"Tulipofungwa mechi ya kwanza, tulifanye 'review' kuona ni wapi tulikosea, tulirekebisha makosa na kupata ushindi kwenye mechi ya pili na tukaenda 'game three' nma kushinda pia," amesema.

VBC ilishinda mechi 10 na kufungwa tano kwenye Ligi, matokeo yaliyoifanya imalize ya tano kwenye msimamo na kufuzu kucheza nane bora sanjari na JKT, Oilers, Kurasini Heat na ABC ambazo zimefuzu kucheza nusu, huku Savio, Ukonga Kings na Pazi zikiondoshwa sanjari na VBC.