Chui yatoa kipigo, Savio, Pazi kazini RBA

Muktasari:

Mechi nyingine za leo jumapili DTB inacheza na UDSM Outsiders, Magnets inacheza na Ukonga Kings wakati maafande wa Jeshi Stars wakiikabiri JKT Stars upande wa wanawake.

WAKATI mashabiki wakisubiri kuona kama Savio atavunja rekodi ya Pazi kwenye Ligi ya mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam (RBA), Chui imeondoka na pointi mbili baada ya kuichapa Mabibo Bullet leo Asubuhi.

Chui imeifunga Mabibo kwa pointi 73-59 katika mchezo huo wa mzunguko wa saba wa RBA inayofanyika kwenye uwanja wa Bandari, Kurasini.

Ushindi huo unaifanya kufikisha pointi 12 katika mechi saba ilizocheza ambapo imefungwa mbili na kushinda mechi tano huku ikikamata nafasi ya 10 katika msimamo.

Mbali na mechi hiyo, mashabiki wa RBA wanasubiri mchezo wa saa 2 usiku kati ya vigogo, Pazi dhidi ya Savio uwanjani hapo.

Pazi itaikabili Savio ikiwa na rekodi ya kutofungwa katika Ligi hiyo tangu msimu huu uanze sanjari na JKT ambayo imecheza mechi saba.

Kama itapoteza mchezo huo, itakuwa ni mechi ya kwanza Pazi kufungwa katika mechi zake saba za msimu huu na Savio ambayo mpaka sasa imecheza mechi sita na kufungwa mbili ikivunja rekodi hiyo.