Chirwa afichua beki kisiki yupo Yanga tu!

Friday November 9 2018

 

By Charity James

Dar es Salaam. Saa chache baada ya kukamilisha usajili wa kujiunga na Azam, Obrey Chirwa, amemtaja Kelvin Yondani ndiye beki bora anayemnyima usingizi.

Chirwa ametia saini mkataba wa mwaka mmoja kujiunga na Azam baada ya jaribio la kurejea katika klabu yake ya zamani Yanga kugonga mwamba.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Zambia, alisema Yondani ni beki imara ambaye anamuhofia wakikutana katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Chirwa aliyekuwa akicheza No-goom El Mostakbal ya Misri kabla ya kuvunja mkataba, alisema amerejea nchini kuzipa changamoto Simba na Yanga.

"Nimekuja Azam kwa kazi moja kuhakikisha napambana kuisaidia kutwaa ubingwa msimu huu nikiwa miongoni mwa wachezaji watakaofunga mabao mengi katika timu yangu mpya," alisema Chirwa.

Chirwa alisema ana imani Azam itakuwa moto mkali baada ya kuungana na Donald Ngoma ambaye waliwahi kucheza Yanga.

"Nimecheza na Ngoma miaka sita tumekutana Yanga tumecheza kwa mafanikio makubwa nina imani juhudi tulizofanya kule zitaongezeka hapa Azam," alisema mchezaji huyo.

Kocha wa Azam Hans Van der Pluijm alisema ni fahari kwake kukutana na mchezaji huyo na anatambua uwezo wake akiwa ni mshambuliaji mwenye kiwango bora.

"Chirwa ni mchezaji mzuri anajituma uwanjani ana kasi ya kucheza ni mtu mwenye jicho la kuona zaidi goli nina amini ataongeza chachu ya ushindani katika kikosi,” alisema Pluijm.

Kocha Mshindo Msolla alisema Azam imefanya uamuzi sahihi kumsajili Chirwa kwa kuwa ataziba pengo la Ngoma aliyedai hayuko fiti kutokana na majeraha.

 

 

Advertisement