Chirwa: Yondani ni beki katili kwangu

Muktasari:

Obrey Chirwa ni mchezaji aliyeichezea Yanga kwa mafanikio makubwa na kuisaidia timu hiyo kutwaa mataji mawili mfululizo sasa ameungana na Azam FC na kuuahidi makubwa.

ACHANA na Simba na Yanga ambazo zimekuwa zikitawala soka la Bongo, lakini msimu huu Azam ambao walianza kuonekana kama wamepotea vile, wamepania kuzishikisha adabu klabu hizo kongwe.
Ukiachana na Simba ambayo inatajwa kuwa na safu matata ya ushambuliaji ikiongozwa na Emmanuel Okwi, Meddie Kagere, John Bocco na Adam Salama ama Yanga yenye Herieter Makambo, Deus Kaseke, Mrisha Ngassa na Ibrahim Ajibu huko Azam FC kuna mashine za maana kwelikweli hapo mbele.
Iko hivi. Jana Jumatano mabosi wa Azam FC wametangaza kumnasa straika wa zamani wa Yanga, Obrey Chirwa ambaye alitua nchini kwa ajili ya kumalizana na mabosi wa klabu yake hiyo ya zamani, lakini Kocha Mwinyi Zahera akazuia usajili wake.
Wakati Zahera akiweka msimamo wa kutorejea kwa Chirwa, mabosi wa Azam walikuwa wakisubiri kwa pembeni na sasa wamefanya kweli na kumjumuisha Mzambia huyo kwenye kikosi chao na sasa anakwenda kucheza na pacha wake waliokuwa pamoja Yanga, Donald Ngoma. Mbali na Ngoma, Chirwa pia atakwenda kucheza sambamba na Ramadhani Singano (Messi), Enock Agyie, Tafadzwa Kutinyu, Yahaya Zayd na Joseph Mahundi ambao wote wanasimama jirani na lango la adui.
Chirwa, ambaye amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Azam, amefunguka kuwa hajarejea Ligi Kuu Bara kizembe bali ametua kufanya kazi na kuzipa changamoto Simba na Yanga kwenye mbio za ubingwa.
Pia, ameonya kuwa kwa sasa katika Ligi Kuu Bara kuna beki mmoja tu ambaye anaweza kumsumbua katika harakati za kupasia nyavuni pale Yanga, Kelvin Yondani.
Akizungumza baa da ya kusaini mkataba huo, Chirwa amemtaja Yondan kuwa ndiye beki bora kwa sasa na ni pekee anayeweza kumsumbua kwa sasa ana nguvu na anacheza soka la akili hivyo, ni ngumu sana kumpita kirahisi.
Chirwa, ambaye alikuwa akiichezea klabu ya No-goom El Mostakbal FC baada ya kuondoka Yanga, ameachana na klabu hiyo kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya mkataba ikiwemo kutomlipa mshahara.
"Nimekuja Azam FC kwa kazi moja tu ya kufanya kazi na kupambana kuisaidia kutwaa ubingwa msimu huu na kufunga mabao mengi ili kuiweka timu mahali pazuri.
"Sijatua Azam kumaliza soka langu, hapa ni kama njia tu kwa sababu nina mpango wa kutoka tena kwenda kujaribu soka la kulipwa nje ya Tanzania. Mipango yangu ni kucheza soka sehemu ambayo nilishawahi kucheza hapo nyuma, najua wengi hawafahamu niliwahi kucheza na Emmanuel Okwi klabu moja," alisema.
Chirwa alisema kitu kingine kinachompa jeuri ya kuamini ana uwezo wa kufanya hayo yote ni kwenda kucheza pamoja na Ngoma, ambaye walikuwa wote Yanga kwa miaka sita kabla ya kuondoka kwenda Azam.
"Nimecheza na Ngoma kwa mafanikio pale Yanga kwa miaka sita, nina imani juhudi tulizozifanya kule zitaongezeka zaidi hapa Azam kutokana na kuwa na kila kitu kinachotakiwa kwa mchezaji hivyo, tutafanya makubwa zaidi," alisema.
Naye Kocha wa Azam FC, Hans Van Pluijm alisema anafura kubwa kuungana tena na Chirwa kwani, anatambua uwezo wake na ataisaidia Azam kuongeza kasi ya kupasia nyavuni.
"Chirwa ni mchezaji mzuri, anajituma uwanjani na ana kasi. Ni mtu mwenye jicho la kuona zaidi goli hivyo ninaamini ataongeza chachu ya ushindani katika kikosi changu ikiwa ni pamoja na kuisaitia timu kufikia malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu," alisema.
Kwa upande wake, kocha msomi Dk. Mshindi Msolla alisema ujio wa Chirwa ndani ya Azam ni uamuzi sahihi kwani, Ngoma ametoka kwenye majeruhi hivyo bado hana kasi ya mapambano.
"Ngoma kwa sasa anacheza kiujanja ujanja huwezi kumfananisha na yule aliyekuwa moto Yanga, nadhani bado hajapona majeraha yake, Chirwa ni mtu sahihi na atawasaidia," alisema.

WAZIRI JR
Ujio wa Chirwa unamlazimisha Pluijm kuachana na mastraika wake vijana Waziri Jr na Mbaraka Yusuf, ambao wanaweza kupelekwa kwa mkopo kwenye timu ambazo zitawapa nafasi ya kucheza.
Mholanzi huyo alisema kwamba, kuna timu mbalimbali za ndani na nje ya nchi zinahitaji huduma za wachezaji hao, lakini kwa sasa Waziri Jr ndio atatolewa kwa mkopo huku Mbaraka akiendelea kubaki klabuni hapo.

Mashabiki watofautiana
Baadhi ya mashabiki wa Yanga wamepigwa butwaa baada ya Chirwa kutua zake Azam FC wakisema kuwa, mabosi wao wameacha silaha imekwenda kwa adui.
Pia, wameonekana kumtupia lawama Zahera, ambaye aligomea Chirwa kurejea kikosini hapo kwa madai ya utovu wa nidhamu ikiwemo kugoma kucheza wakati timu ikiwa kwenye wakati mgumu msimu uliopita, jambo ambalo halikumfurahisha.
Katibu wa Yanga Tawi la Arusha, Destrich Kateule alisema walitegemea Chirwa angerudi Jangwani kuendeleza makali yake, lakini imekuwa tofauti jambo ambalo wanaamini limetokana na msimamo wa Zahera.
“Kwenye timu kwa sasa hatuna matokeo mazuri, mechi nyingi tumnashinda hivyo hivyo tu na tulitegemea Chirwa angeongezwa kusaidia pale kwenye ushambuliaji, lakini naona hali imekuwa ndivyo sivyo.”
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Athumani Kihamia alisema suala la nidhamu kwa mchezaji ni la msingi na kwamba, Zahera yuko sahihi.
“Kwa hilo sipingani naye kabisa, lakini bado tuna mahitaji kwenye eneo la ushambuliaji kwa sababu timu inalinda zaidi hivyo, kama sio ishu ya nidhamu Chirwa angeweza kutusaidia,” alisema.

Lakini, usajili huo wa Chirwa umeonekana kuwagawa nyota wa zamani wa Yanga, ambao baadhi yao wamedai Zahera alikuwa sahihi kumkataa Chirwa na wengine wakisisitiza kwa mahitaji ya Yanga kipindi hiki, Mzambia huyo alistahili kurejeshwa Jangwani.
"Kwa rekodi ya Chirwa, ni mchezaji ambaye alikuwa akihitajika Yanga tofauti na Azam, lakini nadhaniu washauri wa Zahera hawakumshauri vizuri kuhusu Chirwa," alisema Ally Mayay ambaye pia ni mchambuzi wa soka.
Alisema Zahera hakuwahi kumuona Chirwa, ndiyo sababu alimkataa, lakini kwa mahitaji ya klabu, bado Yanga ilimhitaji mchezaji huyo na hatua ya Pluijm kumsajili ni kwa sababu anamfahamu vizuri.
Alisema Chirwa alikuwa sahihi kuanzisha sekeseke la kudai mshahara wake Yanga, kwani tofauti na wachezaji wa nyumbani, yeye amekuja nchini kucheza ili alipwe, hana uzalendo hivyo madai yake yalikuwa ya msingi.
Hata hivyo, Mayay amepingwa kwa nguvu zote na nyota wenzake wa zamani wa timu hiyo, Abed Mziba na Peter Tino ambao wamedai Yanga ni kubwa kuliko Chirwa, hivyo sio timu ya kubembeleza mchezaji.
"Chirwa haijui historia ya Yanga, iliwahi kuwaacha wachezaji wa kikosi kizima mwaka 1970, wachezaji ambao walikuwa na majina kweli kweli, hata wakitajwa nchi inatikisika akiwamo Sunday Manara, waliondoka na Yanga ikaendelea kuwepo, sembuse Chirwa, wacha aende tu Azam," alisema Mziba.
Alisema Klabu haiwezi kumbeleza mchezaji, huku akidai Chirwa hana jambo jipya ambalo anadhani mchezaji chipukizi wa Yanga ataiga kupitia kwake.

Upande wa Tino alisema kitendo cha kocha kumkataa Chirwa hata yeye angekuwa kiongozi angefanya hivyo kwani, kitendo cha kususia timu hakikutoa taswira njema.
"Yanga ni timu ambayo mchezaji akisumbua wanaachana naye hilo wanaliweza, Chirwa kabla ya kuondoka Yanga angekumbuka namna alivyotua nchini, jinsi Yanga ilivyompokea na kumpa nafasi, kipindi kile kilikuwa cha mpito Yanga, lakini hakuvumilia," alisema.