Chirwa: Sasa naitaka ile Yanga ya akina Makambo

Muktasari:

Mzambia Obrey Chirwa alisajiliwa na Yanga, Julai 2016 na aliichezea kwa mafanikio, lakini ukata kwenye timu hiyo ulimfanya atimkie
nchini Misri na kujiunga na Nogoom FC, Julai 17 mwaka jana.

Zanzibar. Mfungaji wa mabao mawili ya Azam dhidi ya Yanga kwenye Kombe la Mapinduzi, Obrey Chirwa amesema nafsi yake itasuuzika atakapoifunga na Yanga iliyobaki Dar es Salaam.
Chirwa aliyasema hayo baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya Yanga juzi kwenye Uwanja wa Amaan ikiwa ni mfululizo wa
mashindano ya Kombe la Mapinduzi. Bao lingine lilifungwa na
Enock Atta na Azam kushinda 3-0.
“Kwa mimi ni kama sihesabu, kipimo chetu ni kucheza na Yanga iliyopo Dar es Salaam, hawa tumecheza nao ni watoto ingawa uwezo wao upo juu,  wanacheza vizuri sana na wanastahili pongezi japokuwa wameshindwa kufunga,” alisema Chirwa.
Yanga imepeleka kikosi cha pili Kombe la Mapinduzi na Chirwa
alisema: “Nimefunga na mimi sikujisikia kushangilia kwa kuwa
ninakitaka kile kikosi cha akina Makambo (Heritier) kilichobaki
Dar es Salaam, pale ukifunga huwezi kuacha kushangilia.
“Nitafurahi kuifunga Yanga iliyobaki Dar es Salaam maana ndiyo yenye ushindani na ndicho kitakuwa kipimo changu.
“Huu ni mpira lolote linaweza kutokea, ila nitafurahi tukicheza na Yanga iliyobaki Dar niwafunge na ninaamini nitawafunga tu.”
Alisema Yanga sio timu mbaya hata hawa waliocheza ni wazuri
sana.
“Mpira unabadilika na mimi ninaangalia masilahi unaweza kesho ukanikuta nimerudi Yanga ama nimekwenda Simba yote haya ni kutafuta maisha.”
Chirwa alisema pia ubingwa wa ligi bado hauna mwenyewe Yanga,  Simba na Azam mmoja wapo anaweza kutwaa ubingwa, kikubwa ninachoweza kusema kuhusu Yanga nawaombea mafanikio kwani ni timu niliyoichezea,” alisema Chirwa
Mzambia huyo alisajiliwa na Yanga, Julai 2016 na aliichezea kwa mafanikio, lakini ukata kwenye timu hiyo ulimfanya atimkie
nchini Misri na kujiunga na Nogoom FC, Julai 17 mwaka jana.
Hesabu zake zilienda ovyo nchini humo kutokana na kutopewa fedha zake za usajili na alirejea Tanzania ili ajiunge na Yanga lakini
kocha, Mwinyi Zahera aligoma kumpokea licha ya baadhi ya
viongozi kumpigia debe, ndipo Azam ilipoamua kumnasa
mshambuliaji huyo.
Azam ilimsajili Chirwa Novemba 8, mwaka jana na alitoa ahadi ya kufanya kila awezalo kama mshambuliaji kuhakikisha ‘Wanalambalamba’ hao wanafikia malengo yao kwenye msimu huu.
Naye Meneja wa Yanga, Nadir Haroub alisema baada ya mchezo wa juzi: “Bao la kwanza tunamlaumu mwamuzi hakutenda haki, bao la pili na tatu tunakiri ni uzembe wa mabeki na kipa.
“Tuliingia na malengo ya kucheza sana pembeni ili tupate matokeo baada ya kuwasoma wapinzani wetu lakini mpango huo ulifeli.
“Lakini mpira ndivyo ulivyo na tunakubaliana na hayo yote
tunajipanga kwa ajili ya mechi ijayo, wapinzani wetu wamefanikiwa mipango yao na wamecheza vizuri kutimiza lengo,” alisema.