Chelsea yatakata ugenini

Muktasari:

Chelsea jana ilicheza mechezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu, England dhidi ya Brighton na ikaibuka na ushindi wa mabao 3-1.

LONDON, ENGLAND. KIMEWAKA pale kwa Malkia, Ligi Kuu England iliendelea jana Septemba 14, 2020 kwa michezo miwili ambapo mchezo wa mwisho ulikuwa kati ya wababe wa Jiji la London, Chelsea iliyoumana na Brighton & Hove Albion na imefanikiwa kushinda mabao 3-1.

Chelsea ilijipatia bao la kwanza kwa penati iliyopgwa na Jorginho kabla ya Brighton kuchomoa dakika  ya 54 kupitia kwa Leandro Trossard, lakini Chelsea ilikuja kuongeza bao la pili dakika mbili baadae kupitia kwa Reece James.

Dakika ya 66, Kurt Zouma alipigilia msumali wa mwisho uliopoteza matumaini ya Brighton kupata ushindi katika kiwanja chake cha nyumbani.

Baada ya mchezo huo Chelsea inakuwa imeweka rekodi ya kufunga mabao 42, ya ugenini tokea kuanza kwa msimu uliopita, ambapo inakuwa ni timu ya pili kuwa na idadi kubwa ya mabao nyuma ya Manchester City ambayo ina mabao 45.

Huku upande wa golikipa wa miamba hiyo Kepa Arrizabalaga ameweka rekodi ya kufungwa mabao mengi kutokea nje ya boksi kuliko kipa yeyote katika Ligi Kuu, England, tokea ajiunge na Chelsea mwaka 2018, kiujumla amefungwa mabao 19.

Mpigaji penati wa Jorginho ameweka rekodi ya kupata penati zote ambazo amekabidhiwa apige kwenye michuano yote, akiwa amepiga jumla ya penati nane na tano kati ya hizo ni za Ligi Kuu, na zilizobakia ni katika michuano mingine, lakini rekodi hiyo haihusiani na ile ya penati alizopiga baada ya mechi.

Mchezo wa mapema uliozikutanisha Sheffield United na Wolverhampton Wanderers, Wolves ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 na imepaa hadi nafasi ya tano, huku Chelsea nayo imepanda hadi nafasi ya tatu.