Chelsea na Messi iko hivi

LONDON, ENGLAND. UMESIKIA hii? Chelsea imeripotiwa kwamba ishajiweka sawa na kukubali kumlipa supastaa Lionel Messi mshahara wa Pauni 1 milioni kwa wiki ili atue kwenye kikosi chao wakati ilipotenga ada ya Pauni 225 milioni kumsajili mwaka 2014.

Bilionea mmiliki wa klabu ya Chelsea, Roman Abramovich alikuwa tayari kuzama mfukoni na kutoa mkwanja mrefu kunasa huduma ya supastaa huyo wa Kiargentina baada ya kocha Jose Mourinho kumpigia simu staa huyo, kwa mujibu wa Gianluca di Marzio wa Sky Italy.

Bilionea huyo wa Russia pamoja na kocha Mourinho walikuwa tayari kutoa mkwanja wa kuvunja mkataba wa Messi na ilikuwa tayari kutoa mshahara wa Pauni 50 milioni kwa mwaka.

Ripoti zinadai kwamba Chelsea mara ya kwanza ilifanya mawasiliano na Messi Januari 2014 baada ya kesi yake ya mambo ya kodi. Staa huyo alionyeshwa kuchoshwa na mamlaka za kodi za Hispania na jambo hilo liliwafanya The Blues kuamini kwamba wangeweza kutumia kama fursa ya kunasa saini yake.

Messi alimuuliza rafiki wake wa zamani klabuni Barcelona, Deco kuhusu mtazamo wake wa kwenda kucheza Stamford Bridge, kabla ya kupigiwa simu kwa njia ya video na kocha Mourinho kupitia FaceTime.

Messi anaripotiwa kwamba alishawishiwa na Mourinho kwenye mazungumzo hayo na alikuwa tayari kwenda kukipiga katika kikosi cha The Blues na mambo yanadaiwa yalirahisishwa zaidi na Deco kabla ya Mourinho kuzungumza moja kwa moja na Messi.

Cesc Fabregas - ambaye pia alikuwa akielekea Chelsea kwenye dirisha hilo la majira ya kiangazi, naye alimwambia Deco, ambaye alikwenda kumshawishi moja kwa moja baba yake Messi, Jorge, ambaye alichukia kusikia Mourinho aliongea na Messi.

Di Marzio alifichua hilo kupitia kitabu chake, Grand Hotel Calciomercato, ambapo alisema pia Real Madrid walijaribu mpango wa kumsajili Messi mwaka 2013. Lakini, Muargentina huyo hakuwa tayari kuhamia kwa mahasimu wao hao wa El Clasico.

Kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka huu, Manchester City ilijaribu kunasa huduma ya Messi ambapo ilimwaandalia mshahara wa Pauni 2.4 milioni kwa wiki. Staa huyo yupo kwenye mwaka wa mwisho wa mkataba wake huko Nou Camp.