Cheki dili la winga Mtanzania FC Porto

MTANZANIA Orgenes Mollel amefunguka kuwa alipotoka katika Akademi ya Aspire ya nchini Senegal, alikwenda kufanya majaribio katika klabu ya FC Porto ya Ureno.

Winga huyo, ambaye kwa sasa anaichezea Bairro FC ya nchini humo, alisema alifuzu majaribio hayo na FC Porto ilitaka kumsajili kwa bahati mbaya wakala wake alitaka pesa nyingi za usajili wake kutoka FC Porto.

Jambo ambalo lilimfelisha kujiunga na miamba hiyo ya Ureno, baada ya hapo akatimkia katika klabu ya Famalicao ya Daraja la Pili.

“Alionyesha tamaa wakala wangu ndio maana ilishindikana kujiunga na FC Porto, sikuwa mchezaji wa daraja la pesa ambayo alitaka pamoja na kuwa umri wangu ilikuwa mdogo. Niliumia sana, ikabidi nikubaliane na kilichotokea na kusonga mbele,” alisema.

Molllel, 22, anaamini kuwa bado ana nafasi ya kufika mbali zaidi ambapo hadi sasa amepata ofa kadhaa za timu za Ligi Kuu barani Ulaya ambazo anaamini msimu ujao atacheza moja ya klabu hizo.

“Nimeona kuwa Ligi zimeanza kurudi ni jambo jema, utakuwa wakati mzuri kwangu kumalizia msimu na kuangalia wapi naweza kuwa msimu ujao,” alisema winga teleza huyo mzaliwa wa Dodoma.