Chambua: Serengeti Boys wasahau ya Uturuki, Afcon yao

Muktasari:

  • Tanzania mwenyeji wa mashindano ya Afcon yanayoanza Aprili, mwaka huu na Serengeti Boys iko kundi A ikiwa na timu za Nigeria, Angola na Uganda.

Dar es Salaam.Mchezaji wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua amesema licha ya timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 'Serengeti Boys' kutolewa mapema katika mashindano ya UEFA Assist kule Uturuki, bado ina nafasi ya kufanya vizuri kwenye Afcon inayoanza kutimua vumbi mwezi ujao nchini.

Ikiwa nchini Uturuki, Serengeti Boys ilicheza mechi tatu na kushinda mmoja huku ikipoteza miwili mbele ya Guinea kwa kuchapwa bao 1-0 kisha wakaichapa Australia mabao 3-2 na baadaye kumaliza na Uturuki na kufungwa mabao 5-0.

Chambua alisema maandalizi ya Serengeti Boys nchini Uturuki ni kipimo kizuri na wanaweza kuyatumia kama changamoto kwa kufanyia kazi mapungufu waliyojitokeza kabla ya mashindano hayo.

"Uturuki wamekutana na timu zinamaandalizi mazuri na makubwa zaidi yao wamepewa changamoto kwa kufungwa na kutolewa mapema hivyo ni muda wa mwalimu kutumia makosa aliyoyaonyesha kwa kuhakikisha anayasawazisha kabla hawajaanza mashindano ya Afcon na wao wakiwa kama wenyeji.

"Tuna timu nzuri inapambana na inafundishika naamini bado tunanafasi nzuri ya kutumia vizuri uwanja wetu wa nyumbani kwa kutwaa taji la mashindano hayo watanzania tunatakiwa kuungana pamoja kuwapa ushirikiano wachezaji wetu ili waweze kufanikisha hili,' alisema.

"TFF na benchi la ufundi wanatakiwa kuwaanda kisaiokolojia hawa vijana na kuwaanimisha kuwa, kutolewa kwao mapema sio hatua mbaya wala njia ya kufanya vibaya kwani, wao bado ni bora uwanjani," alisema.

Tanzania mwenyeji wa mashindano ya Afcon yanayoanza Aprili, mwaka huu na Serengeti Boys iko kundi A ikiwa na timu za Nigeria, Angola na Uganda.