Chama balaa!

Muktasari:

Utulivu uwanjani, nidhamu na kujitambua ndio zinambeba sana.

BEKI wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa amefichua kitu kinamchofanya kiungo, Clatous Chama kuendelea kuwa na heshima mbele ya mashabiki.

Amesema utulivu uwanjani, nidhamu na kujitambua ndio zinambeba sana.

Alisema Chama ni mjanja wa kusoma alama za nyakati na kujua mashabiki wa Simba wanataka nini kwake na ndicho anachokifanya hivyo, inakuwa ngumu kumshusha thamani yake. Kiuwezo alisema Chama ni mtulivu uwanjani, jambo linalomsaidia kuwa na maamuzi sahihi ya kutumia akili anapokuwa na mpira mguuni, hivyo huduma yake inakuwa ya muhimu katika timu yake.

“Mchezaji hata kama una uwezo kiasi gani, lakini ukiwa na nidhamu mbovu na kazi huwezi kufika popote, nilichokiona kwa Chama wakati wa kazi akili yake inakuwa kwenye kazi ndio maana si mchezi anayechosha kumuangalia anapocheza.

“Napenda kumtolea mfano Mbwana Samatta, ambaye amejitambua na kujijua yeye ni nani katika soka na ndio maana anapiga hatua mbele, hivyo kwa upande wa Chama amejua soka la Tanzania linataka nini,” alisema.

Kocha msaidizi wa Gwambina FC, Athuman Bilali ‘Bilo’ alisema Chama ni miongoni mwa wachezaji wakigeni ambao, wanamvutia kiuchezaji na anachokipenda zaidi ni utulivu ambao, unamfanya asipoteze mipira kizembe.

Adam Salamba anayecheza soka la kulipwa nchini Kuwait katika klabu ya Al-Jahra SC ya Daraja la Kwanza, alisema; “Nilichojifunza kwa Chama ni kutofautisha maisha yake ya kazi na nyumbani, naamini hilo linamsaidia kuendelea kuwa kwenye ubora wa juu na thamani mbele ya mashabiki wa Simba.”