Cavani kuikosa Newcatle, PSG

MANCHESTER, ENGLAND. MASHABIKI wa Manchester United bado hawana uhakika na chama lao baada ya kupewa kipigo cha mabao 6-1 na Spurs, baada ya kushindwa kufanya kweli kwenye soko la usajili.

Hata hivyo, ujio wa straika mpya Edinson Cavani na beki wa pembeni Alex Telles kidogo ukawapa matumaini ya kurejea kwenye ubora wao, lakini taarifa hizi mpya ni kama zimewapa wasiwasi.

Ndio, Manchester United ya Ole Gunnar Solskjaer inakabiliwa na mechi ngumu ikiwemo dhidi ya Newcastle United kwenye Ligi Kuu England kisha itakipiga na wababe wa Paris, PSG kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini, kwenye mechi hizo inaweza kuingia uwanjani bila huduma ya Cavani kutokana na taratibu za kujikinga na virusi ya corona zilizowekwa na Serikali ya Uingereza.

Ipo hivi, Cavani amewahi kukutwa na maambukizi ya virusi vya corona, hivyo sheria inamtaka kukaa karantini kwa wiki mbili kabla ya kujiunga na timu, hivyo atalazimika kujiweka pembeni hadi Oktoba 19. Hata hivyo, mabosi wa Man United wanapambana kuona kama anaweza kujiunga na wenzake kabla ya muda huo ili kuwahi mechi hizo.

Hivi karibuni Cavani na mchumba wake walikutwa na maambukizi ya virusi hivyo wakati walipokwenda kula bata huko fukwe za Ibiza.

Kama mambo yatakwenda kama United wanavyopanga basi Cavani atauwahi mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya chama lake la zamani, PSG.