Carlinhos atawaua, mipasi kama De Bruyne, faulo kama penalti

MASHABIKI wa Yanga huwaelezi kitu kuhusu staa mpya, Carlos Carlinhos na jana wakamteua kuwa mchezaji bora wa mechi yao na Mbeya City ya Kocha Amri Said, ambaye ni beki wa zamani wa Simba.

Carlinhos ambaye awali baadhi ya mashabiki walikuwa na shaka na kiwango na ufiti wake, alipata asilimia 44 ya kura za mashabiki akiwashinda mastaa kibao akiwemo straika Mghana Michael Sarpong.

Kocha wa Yanga, Zlatko Krmpotic alisema Carlinhos ambaye ni mchezaji pekee wa kigeni kuwahi kupata mapokezi makubwa zaidi alipotua Bongo kuliko staa, ni mchezaji wa kiwango cha juu lakini, bado hajaiva kama inavyotakiwa licha ya kuisaidia timu yake kupata ushindi wa kwanza kwenye Ligi Kuu Bara. lakini bado hajaiva asilimia zote.

Miongoni mwa sifa za kiufundi zilizombeba Carlinhos juzi ni kupiga pasi za mbele zenye umakini, faulo za hatari, kona zenye macho na mashuti makali langoni.

Zlatko alisema Carlinhos alitumia akili, ufundi na kipaji kuamua matokeo ya mchezo huo ambao ulionekana kama Yanga inakwenda kupata sare nyingine. Katika mchezo huo baada ya kuingia dakika ya 68, Carlinhos alitengeneza nafasi zaidi ya ya tatu za kufunga, lakini wenzake walishindwa kumaliza kazi.

“Unajua Corlinhos ana uwezo na kipaji ila hakucheza mpira kwa muda mrefu kutokana na ligi kusimama kwa sababu ya corona, nahitajika kupata muda zaidi wa kumuandaa.

“Nikisema nimuandae kwa nguvu ili nimtumie haraka nitakuwa kama nataka kumuumiza, lakini taratibu atakuwa anapata muda wa kucheza na ataonyesha kiwango bora zaidi ya hiki,” alisema Zlatko, ambaye bado hajapata muunganiko mzuri wa kikosi cha kwanza Yanga.

Katika mechi hiyo ambayo Mbeya City walitaka kufuta aibu ya mabao 4 waliyopigwa awali na KMC, walishindwa kuendana na kasi ya Yanga hasa kipindi cha pili.

“Bado kutakuwa na mabadiliko machache kulingana na maandalizi ambayo tutafanya mpaka kupata kikosi ambacho kitakuwa imara na kufanya vizuri zaidi.

“Mbali ya mabadiliko, pia kuna mapungufu kama Mukoko Tonombe alionyesha udhaifu katika kukaba, Tuisila Kisinda kuna wakati alicheza chini ya uwezo wake jambo ambalo tutalifanyia kazi,” alisema Zlatko anayeikabili Kagera Sugar ugenini wikiendi ijayo.

Katika hatua nyingine Zlatko alisema alilazimika kutumia mastraika watatu kwa pamoja kutokana na uimara walionyesha wapinzani wao na atakuwa akifanya hivyo katika mechi za aina hiyo.

Zlatko, ambaye ana uzoefu na soka la Afrika, alisema miongoni mwa silaha zake anapokutana na mechi ngumu ni mastraika watatu Sarpong, Yacouba Sogne na Ditram Nchimbi kuwatumia kwa wakati mmoja.

“Ni hatari kutumia mastraika watatu kwa pamoja kwani, lolote linaweza kutokea ila hakuna jinsi kama unataka matokeo na mambo sio rahisi. Uliona mambo yalibadilika na tukapata matokeo sahihi,” alisema Zlatko aliyewahi kuinoa TP Mazembe iliyobeba ubingwa wa Afrika.

“Walikuwa bora katika kupambana hawakati tamaa, hiyo ni nidhamu bora walijaribu kila hatua na kuwaweka wapinzani kwenye presha.

“Tuna watu ambao wanajua timu inataka nini, hata kama inaamua kujilinda lakini uhakika wa kupata kile mnachotaka unakuwepo, kama nashambulia kwa nguvu mna uwezo wa kupata mabao tu,” alisema.

Kocha wa Mbeya City Amri Said ‘Stam’ amesema Yanga ya msimu uliopita na hii ya sasa ina tofauti kubwa.

Stam, ambaye alikuwa beki wa mafanikio wa Simba miaka ya nyuma alisema Yanga sasa ina kikosi imara ambapo, wachezaji wengi wana ubora wa kujua kutengeneza nafasi na kupambana kutafuta matokeo bora ndani ya uwanja.