Carlinho kuwakosa Polisi Tanzania

Muktasari:

Mchezo wa Yanga dhidi ya Polisi Tanzania unatachezwa saa 10:00 jioni katila Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

KIUNGO Carlos Fernandes 'Carlinho' wa Yanga ataukosa mchezo wao wa Alhamisi dhidi ya Polisi Tanzania kutokana na kusumbuliwa na majeraha.

Carlinho alianza kukosekana katika mazoezi ya Jumapili pamoja na  Abdulaziz Makame, Balama Mapinduzi na Fahad Fuad, lakini wenzake hao pia walionekana uwanjani hapo.

Katika mazoezi ya leo Jumanne Carlinho ameendelea kukosekana kabisa katika mazoezi hayo huku Abdulaziz Makame ameanza kufanya mazoezi mepesi, Fahad Fuad akichangamana na wachezaji wenzake wakati huo huo Balama yeye akiwa bado hajawa fiti.

Baada ya mazoezi kumalizika Mwanaspoti lilizungumza na kocha wa Yanga, Cedrick Kaze kutaka kufahamu ya hali ya Carlinho ndipo alisema hatokuwa sehemu ya mchezo wao.

"Carlinho anaumwa na ndio maana amekosekana katika mazoezi yetu, amepewa ruhusa na daktari wetu kwanza apumzike, aliumia katika mazoezi wiki iliyopita."

"Katika michezo yetu ya ugenini tukiwa tunasafiri, anaweza akawa tayari ameshakaa sawa na kuwa sehemu ya kikosi chetu."

Akizungumzia hali ya wachezaji wengine waliokuwa majeruhi alisema "Makame alikuwa anasumbuliwa na Malaria lakini tayari ameshaanza mazoezi mepesi , Fahad yupo sawa lakini Mapinduzi ni majeraha ya muda mrefu na anapona pole pole."

Cedric aliongeza kwa kusema hali za wachezaji wengine zipo sawa kwaajili ya kuwa sehemu ya mchezo huo.

 

Imeandikwa na Thomas Ng'itu, Olipa Assa na Eliya Solomon.