Bwalya, Sogne sasa rasmi Yanga

Mabingwa wa kihistoria Tanzania, Yanga imeendelea kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao kwa kumsajili kiungo nyota wa Power Dynamos ya Zambia, Larry Bwalya sambamba na Yacouba Sogne wa Burnikafasso.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zimesema Bwalya, raia wa Zambia, amesaini mkataba wa miaka miwili na kuwa mchezaji wa sita kutua Jangwani tangu dirisha lifunguliwe.

Wengine ni Bakari Nondo Mwamnyeto (Coastal Union), Yasin Mustapha (Polisi Tanzania) na Kibwana Shomari kutoka Mtibwa Sugar ya Turiani.

Pia kuna washambulaji, Junior Waziri kutoka Mbao FC ambayo imeshuka daraja.

Jana, Yanga pia ilimtambulisha Sogne Yacouba aliyekuwa anachezea Asante Kotoko ya Ghana.

Mshambuliaji huyo raia wa Burkina Faso, amesaini mkataba wa miaka miwili.

Bwalya, ambaye anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji akipiga miguu yote, pia anaweza kutumika kama mshambuliaji kutokana na uwezo wa kufunga mbali na kutoa pasi za mwisho.

Habari kutoka ndani ya Yanga ni mchezaji huyo alipaswa kujiunga na wenzake kwenye mazoezi ya timu hiyo yaliyoanza juzi jijini, lakini muda wowote atatua Dar.

“Tumedhamiria kufanya mambo makubwa msimu huu ili kufikia malengo tuliyojiwekea,” alidokeza mmoja wa vigogo wa Yanga huku akisisitiza baada ya kumaliza sakata la Morrison wataweka mambo yote wazi kuhusu usajili mpya.

Pia, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alipoulizwa jana alisema; “Kuna wachezaji wengi wamekwama kuja nchini kutokana na kutokuwepo kwa usafiri wa ndege.

“Wote walitakiwa kuja nchini kabla ya timu kuanza mazoezi. Yacouba ni mchezaji wetu halali kwa sasa kutokana na kusaini mkataba wa miaka miwili, huyo mwingine subiri mambo yakamilike tutaweka wazi.”

Hata hivyo, Mwanaspoti pia linafahamu kuwa tayari Yanga imemalizana na winga wa AS Vita ya DR Congo, Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe ambao wanasubiri anga la nchi yao lifunguliwe ili kuja kuungana na wenzao tayari kwa msimu mpya.