Burundi ni somo kwa nyota wa Taifa Stars

Dar es Salaam. Timu ya Taifa Tanzania inajiandaa kucheza mchezo wa kirafiki wa kalenda ya FIFA na timu ya Taifa Burundi, mchezo utakaochezwa Oktoba 11 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Wakati wakiwa wanajiandaa na mchezo huo,kocha mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije atatangaza kikosi chake Oktoba 2, 2020 kwa ajili ya kuingia kambini.

Timu hizi katika mchezo wao wa mwisho walitoka sare 1-1 kwenye mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia, Qatar 2022 ulipigwa katika Uwanja wa Mkapa, Septemba 8, 2019.

Kwenye kikosi cha Burundi kilichoitwa na kocha wao Jimmy Ndayizeye amewaita nyota 11 wanaocheza nje ya Burundi Saido Berahino (Zulte Waregem- Ubeligiji), Cedric Amissi (Al-Taawoun FC- Saudi Arabia) na Fiston Abdoul Razzak (Fiston), Mohamed Amissi(Heracles Almelo), Philip Nzeyimana (Akademisk Boldklub- Denmark), Fredrick Nsabiyumva (Chippa United- Afrika Kusini), Bimenyimana Bonfils (FK Pohronie- Slovania), Yusuff Nyange Ndayishimiye(Yeni Malatyaspor), Jonathan Nahimana (Namungo), Bigirimana Blaise (Namungo) na Steve Nzigamasabo (Namungo).

Kuwa na wachezaji 11 wanaocheza nje hasa kwenye Ligi bora ndani na nje ya Afrika hii inaonyesha dhahiri kwamba ni kipimo tosha kwa mchezo wa kirafiki katika kalenda ya Fifa.

Kwani mchezo huu unakuwa na mvutano mkubwa katika timu zote kwa sababu kama utapoteza hapa unashuka na kama utashinda basi utapanda katika viwango vya FIFA.

Hadi sasa katika viwango vya FIFA, Tanzania wanashika nafasi ya 38 kwa Afrika na kidunia 134 huku Burundi wao kwa Afrika wakishika nafasi ya 43 na kidunia nafasi 149.

Nyota wa zamani wa Yanga, Zamoyoni Mogella alisema sababu kubwa ya wachezaji wengi wa tanzania kutotoka kwenda kucheza soka la kulipwa nje kama Burundi imetokana na kutojiamini kwao.

Mogella alisema hali hiyo pia imewafanya hata wachezaji wa kigeni kuja nchini na kuendesha soka la bongo kutokana na wachezaji wa Tanzania kulizika na kitu ambacho wanakipata.

“Unajua sisi wachezaji wetu wanaocheza soka la kulipwa la ushindani kwenye klabu zenye ushindani ni Mbwana Samatta (Fenerbahce), Thomas Ulimwengu (Tp Mazembe) na Simon Msuva (Difaa Al Jadida), tofauti na wenzetu hao ukiangalia,” alisema Mogella.

Kwa upande wa mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi, Zamoyoni alisema sio kipimo sahihi kwa Stars kama wanataka kujiweka fiti zaidi kwaajili ya kwenda kushindana katika Mashindano ya mbele.

Kwa upande wa mshambuliaji wa zamani Yanga, Herry Morris amesema utofauti wa wachezaji nchi nyingine za Afrika kuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi zao inatokana na sapoti wanayopewa.

“Unajua wenzetu wanapeana sapoti ya kutosha, mfano hao Burundi makocha wao wanaenda kusomeshwa nje ya nchi, sasa kam kocha anapelekwa kwanini mchezaji pia asipewe sapoti anapokuwa anataka kwenda nje kucheza”.

Akizungumzia upande wa mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi alisema ni kipimo sahihi kwa Stars kutokana na timu hiko kuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa wengi nje ya nchi yao.