Bongo zozo : Ukimuita mzungu hili litakuhusu tu -2

Friday July 12 2019

 

By Khatimu Naheka

JUZI, Jumanne, tulianza kuchapisha makala za shabiki huyu matata wa timu ya taifa, Taifa Stars, Nick Reynolds maarufu kama Bongo Zozo a.k.a Mzee wa Fuzo Zisizoumia.

Shabiki huyo ambaye ni raia wa Uingereza alikuwa mmoja wa mashabiki waliokwenda Misri kuishuhudia Taifa Stars ikipambana kwenye fainali za Afcon 2019 na kutolewa, huku akiwa kivutio kikubwa.

Sababu ya Bongo Zozo kuwa kivutio ni jinsi ambavyo alivyoishangilia Stars, lakini utamu ni matumizi ya lugha ya Kiswahili. Kwa muonekano wake ni vigumu kujua kama anafahamu Kiswahili, lakini jamaa anatema lugha kama amezaliwa Tanzania.

Katika makala iliyopita alieleza alipozaliwa, sababu ya kuja kwake Tanzania na jinsi alivyojifunza Kiswahili baada ya kupendana na Mtanzania waliyeoana na kuzaa watoto wawili, huku akisifia maisha ya Afrika yanayotofautiana na Ulaya. Alifichua kuwa licha ya kwamba kwa sasa anaishi Uingereza, lakini hata akiwa huko huwa anaendelea kukizungumza Kiswahili na hupenda kumchangamkia kila Mwafrika na kumzozea lugha hiyo akio nyesha anavyo ithamini mb ali na kuizimikia Tanzania.

Leo tunaendelea tena na simulizi yake iliyotokana na mahojiano maalumu aliyofanyiwa nchini Misri ambapo anafichua jinsi asivyopenda kabisa kuitwa Mzungu. Kwanini? Endelea naye...!

HAPENDI KUITWA MZUNGU

Advertisement

Ukikutana na Bongo Zozo ukamuita mzungu akikunyamazia kakuheshimu sana, lakini jamaa hataki kabisa kuitwa hivyo na huwa hafichi kumweleza ukweli anayemuita hivyo, na anafafanua kwa nini hapendi.

“Ni kama ubaguzi fulani hivi. Awali wakati nipo Tanzania, nilikuwa najisikia vibaya, nilikuwa nawaambia waniite kaka kwani niliona kama ubaguzi kwa sababu nisingeweza kuwaita weusi, ila baadaye nikaja nikagundua kijijini watoto wanaona ni kitu rahisi kuita hivyo, ila sipendi kabisa.”

Anasema anafurahia sana kuitwa jina lake la Bongo Zozo ama Mzee wa Fujo Zisizoumiza kuliko kuitwa mzungu kwa vile anaona hatendewi haki.

MBOGA YAKE MNAFU

Kuonyesha jamaa anajua vyakula vya asili amenishtua akinitajia chakula anachopenda, hebu msikie!

“Nikiwa Tanzania, huwa napenda mboga ya majani ya mnafu na ugali, yaani hata nikija Tanzania nikaribishwe chakula hicho yaani kama jana (siku ya mahojiano) ilikuwa balaa wakati naingia uwanjani, watu kama 1,000 walikuwa wananivuta huku na kule wapige picha na mimi.

“Kuna kasumba watu wakijulikana wanadharau watu wanakuwa hata hawajibu ujumbe wa watu wanaowatumia, mimi huwa najitahidi kujibu kwa njia ya mtandao, ila nikija Tanzania wengi wananiambia watanipa zawadi, sitaki kikubwa nikija kwako wewe nikipikie ugali na mnafu inatosha sana,” anasisitiza.

AMEIONAJE STARS AFCON 2019

Bongo Zozo alikuwepo Misri akihudhuria mechi mbili za mwanzo za Stars na anafichua alichokiona kwa timu hiyo. “Unajua mwanzo mgumu ndio tumeanza, tupambane tutafika mbali, ila wanacheza vizuri unaona ile mechi ya kwanza? Zile dakika 30 za mwanzo niliona kama tunaweza kushinda baadaye mambo yakabadilika.”

“Ila tulichofanya sasa ni hazina kubwa ya baadaye unajua tukumbuke hatukuwa katika mashindano haya kwa miaka 39 ni kama muda huo tulipanda mbegu ambazo zimeanza kuchipua sasa.”

Nini sasa kifanyike ili Tanzania iwe bora kisoka? Bongo Zozo anafunguka, “ tuanze misingi kwa watoto ambao watakuja kufanya vizuri, baada ya miaka sita mbele watapata wachezaji wazuri sana, kama wakichanganyika na hawa baadhi wanaocheza sasa.”

AKWEPA VIGOGO

Kuhusu wito wake na timu anayoshabiki hapa nchini, Bongo Zozo anaanza kwa kujibu, “wito wangu kwa serikali ni kwamba iweke nguvu kwa watoto na vijana katika michezo na hasa soka, hao kina Mbwana Samatta na Simon Msuva baada ya miaka miwili, mitatu watakuwa wamezeeka lakini kama tutaweka nguvu kubwa sasa nina imani mambo yatakuwa tofauti baadaye.”

Juu ya ushabiki wa soka kwa ngazi ya klabu Bongo Zozo anapoulizwa huwa anapenda timu ipi nchini Tanzania, naye anajibu kwa kujiamini. “Napenda kuishabikia Lipuli a.k.a Wanapuluhengo, kuhusu hizo Simba na Yanga sitaki kuchukiwa na upande wowote, timu zote huwa zinacheza vizuri na zina wachezaji bora na ninazipenda.”

Anasema, “nilichogundua ni kwamba nguvu ya mashabiki wa soka Tanzania ipo juu na ilipaswa hata soka lake liwe juu kama nguvu ya mashabiki na hapo nchi ingetikisha duniani.”

Bongo Zozo anakiri ameumizwa kwa Tanzania kutolewa mapema kwenye Afcon 2019, lakini akiamini kama mipango itawekwa vizuri inaweza kwenda tena kwa mwaka 2021.

Je unafahamu anapanga kitu gani kama shabiki wa soka?

Advertisement