Bondia Mtanzania afunguka kuzuiwa kucheza Marekani

Muktasari:

Lyimo ambaye ana rekodi ya kushinda mapambano 23 (15 kwa KO), amepigwa mapambano 12 (7 kwa KO) na kutoka sare mapambano mawili anaishi nchini Marekani kwa zaidi ya miaka minne sasa ambako anafanya kazi na kucheza mapambano.

Dar es Salaam. Bondia Fabian Lyimo ameeleza chanzo cha kupigwa marufuku kuzichapa nchini Marekani.

Lyimo amezuiwa na bodi ya kusimamia ngumi nchini humo ambayo imeeleza kumsimamisha kucheza kwenye mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia.

Akizungumza na MCL Digital kwa njia ya simu kutoka Marekani anakoishi, Lyimo amesema zuio hilo limetokana na kipigo cha KO alichopigwa hivi karibuni.

"Ndiyo utaratibu wa huku  ulivyo, kama bondia umepigwa sana  wanakuwekea pingamizi ili kwamba nchi yoyote utakayokwenda huwezi kucheza kwani rekodi zako zitaonyesha umesimamishwa, ndicho kimefanyika na kwangu," amesema Lyimo.

Amesema tayari ameanza mchakato wa kufuta pingamizi hilo kwa mujibu wa sheria za ngumi nchini humo ambazo kwa sasa ndiko anakoombea kibari cha kucheza mapambano ya ndani na nje ya nchi.

"Moja ya taratibu za Marekani kama umepigwa KO mbaya ni lazima ufanyiwe vipimo kwanza na daktari athibitishe kama huko sawa na unaweza kucheza.

"Hata hivyo, taratibu zote hizo nimefanya na niko sawa na ninaweza kurejea ulingoni, nitakapopeleka vithibitisho hivyo kwenye Bodi ili nifutiwe   pingamizi, ingawa kwa sasa kokote nitakakokwenda siwezi kupigana hadi bodi initolee pingamizi hilo.