Bondia Mkenya aingia mitini Australia

Monday April 16 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Bondia wa Kenya, Brian Agina ameripotiwa kupotea katika kikosi cha wanamichezo wa  nchi hiyo waliowakilisha katika makala ya 21 ya Michezo ya Jumuiya ya Madola yaliyomalizika jana katika jiji la Gold Coast, Australia.

Agina aling'olewa katika michezo hiyo baada ya kupoteza pambano lake katika hatua ya 16 bora dhidi ya Mpakistani, Syed Muhammad Asif.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, Jeshi la Polisi nchini Australia linaendesha msako mkali wa nchi nzima kuhakikisha bondia huyo an anapatika, ingawa Wizara ya michezo ya Kenya bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu kupotea kwa Agina.

Taarifa za kupotea kwa Agina, zinakuja siku chache baada ya kuwepo kwa taarifa za kupotea kwa wanamichezo 13 kutoka mataifa ya Uganda, Rwanda na Cameroon mapema juma lililopita.

Kupotea kwa Agina ni pigo lingine kwa timu ya Kenya, iliyoshiriki katika michezo hiyo, baada ya kushindwa kutamba kama ilivyozoeleka na kumaliza katika nafasi ya 14 kidunia na ya tatu kwa Afrika ikiwa nyuma ya Afrika Kusini na Nigeria.

Katika michezo Kenya ilijizolea jumla ya medali 17, ambazo ni dhahabu 4, fedha 7 na shaba 6. Medali za dhahabu zilipatikana kupitia kwa wanariadha Wycliffe Kinyamal (mita 3000 viunzi), Conseslus Kipruto (mita 3000 viunzi na maji), Hellen Obiri (mita 5000) na Elijah Manangoi (mita 1500).