Bondia Ibrahim Class uso kwa uso na Mayweather Marekani

Muktasari:

  • Japo hapa nchini baadhi ya watu wa ngumi waliibuka na kudai Class amekwenda kuwa ‘sparing patner’ wa bei chee nchini humo na wengine wakidai amekwenda kubeba mabox Marekani, lakini mwenyewe anakwambia huo niuzushi, na siku si nyingi wanaombeza watashangaa.

ULISHAWAHI kufikiria siku moja ukutane uso kwa uso na bondia na mwanamichezo tajiri wa dunia, Floyd Maywether? kama bado, basi sikia kilichomtokea bondia Mtanzania, Ibrahim Class ambaye yuko zake Umangani kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Class bingwa wa zamani wa dunia wa Global Boxig Council (GBC) yuko zake Marekani ambako alipata mkataba na moja ya gym za ndondi nchini humo ambayo inamnoa kwa ajili ya kumwendeleza kipaji chake cha ndondi.

Sasa buana akiwa nchini humo, Class anakwambia walipata fursa ya kuwa miongoni mwa mabondia wa gym yao waliokwenda kufanya mazoezi ya kupigana ana kwa ana (sparing) na mabondia wa gym ya Mayweather iliyopo Las Vegas.

“Ilikuwa ni safari ya faraja kwangu, kwani kwa mara ya kwanza katika historia yangu ya ngumi nilibahatika kumwona laivu Mayweather,” alisema Class alipokuwa akizungumza na Mwanaspoti moja kwa moja kutoka Marekani.

“Alisema maisha ya bondia huyo yamemfanya abadili fikra na kuuchukulia mchezo wa ngumi kuwa si wa kitoto, kwani jamaa ana ulinzi wa kutosha, kana kwamba ni mtu fulani mwenye hadhi kubwa serikalini, lakini kumbe ni sababu ya ngumi.

“Nilipata nafasi ya kumsalimia, lakini sikupiga naye stori, ila alipokuja kwenye gym pale alitueleza mabondia wote tuliokuwa tunafanya mazoezi kuwa tupambane, hata yeye Mayweather alianzia chini, hivyo tukiweka juhudi ngumi zitatutoa,” alisema Class.

Bondia huyo ambaye aliondoka nchini kimya kimya kwenda Marekani anasema kama mambo yatakwenda vizuri, basi maisha yake yanaweza kuwa nchini humo kutokana na mkataba ambao anakwenda kuingia na mmoja wa mapromota wakubwa wa ngumi nchini humo.

Japo hapa nchini baadhi ya watu wa ngumi waliibuka na kudai Class amekwenda kuwa ‘sparing patner’ wa bei chee nchini humo na wengine wakidai amekwenda kubeba mabox Marekani, lakini mwenyewe anakwambia huo niuzushi, na siku si nyingi wanaombeza watashangaa.

Alisema amepata mkataba kuwa chini ya moja ya gym za ngumi ambazo kuna masharti wamewekeana na yanakwenda vizuri na siku si nyingi wataingia mkataba wa muda mrefu kufanya naye kazi na maisha yake yatakuwa nchini Marekani.