Bodi ya Ligi yaibebesha Yanga msala wa Morrison

Muktasari:

Hata hivyo kwa upande wa Viongozi wa Yanga bado wamekuwa wazito kutoa kauli zao na kuishia kurushiana mpira kati yao na kocha.

AFISA Mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo amesema katika kitendo cha winga wa Yanga, Bernard Morrison kuondoka uwanjani moja kwa moja na kuacha kukaa katika benchi, hakuna kanuni yoyote ambayo ina mbana mchezaji wakati anatolewa na kukatazwa kwenda vyumbani.

Akizungumza na Mwanaspoti leo Jumatano Julai 15, 2020 kwenye ofisi za makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kasongo alisema suala la mchezaji huyo kukataa kukaa benchi ni suala la klabu ya Yanga kutolea ufafanuzi kwa sababu ni suala la kinidhamu kwa upande wa klabu.

"Ukitolewa kwa kadi nyekundu tu ndio hauruhusiwi kukaaa katika benchi na muamuzi anaweza akakutoa kama ukataka kukaa katika benchi, lakini Morrison ameshindwa kuwaheshimu mashabiki wa Yanga na hata kocha wake kwa sababu alitakiwa kuwaheshimu na kukaa katika benchi,"

"Kikanuni hakuna inayosema hivyo lakini alitakiwa aheshimu, muamuzi aliyekuwa anamzuia alikuwa anatumia uungwana ili vitu viendelee kama kawaida, lakini alipojaribu kumzuia na kuona kama haelekei alimuacha, alimkumbusha tu" alisema.

Hata hivyo kwa upande wa Viongozi wa Yanga bado wamekuwa wazito kutoa kauli zao na kuishia kurushiana mpira kati yao na kocha.

Morrison baada ya kuondoka uwanjani hapo hakuweza kuhudhulia mazoezi ya Jumatatu na Jumanne ambayo wenzake walifanya wakijiandaa na mchezo wa leo dhidi ya Singida Utd utakaopigwa saa 1:00 usiku.