Bluefins yang’ara mashindano ya kuogelea Mombasa

Monday June 24 2019

 

By Majuto Omary

Dar es Salaam.  Klabu ya Bluefins imeshinda nafasi ya tatu katika mashindano ya kuogelea ya Casa yaliyomalizika jana Jumapili kwenye bwawa la kuogelea la Chuo Cha Bandari, Mombasa nchini Kenya.

Mashindano hayo yalishirikisha jumla ya timu saba na Bluefins ilikuwa timu pekee kutoka Tanzania.

Klabu hiyo imeshinda jumla ya medali 53 na kujipatia pointi 422 katika mashindano hayo. Bluefins ambayo iliwakilishwa na waogeleaji 20, wametwaa medali 18 za dhahabu, 19 za fedha na 16 za shaba.

Klabu ya Bandari iliibuka washindi katika mashindano hayo kwa kupata pointi 1,658 na kufuatiwa na Mombasa Aquatic iliyopata pointi 978. Klabu nyingine zilizoshiriki kaika mashindano hayo ni Otters, Aga Khan Academy Mombasa, Mombasa Parents, Blue Ocean na waogeleaji binafsi.

Muogeleaji Aminaz Kachra (9) aliweza kushinda medali tisa za dhahabu katika mashindano hayo na kuibuka wa kwanza kwa upande wa wanawake wenye umri wake.

Muongeleaji mwingine nyota wa kike, Viva Pujari (7) alishinda medali nne za dhahabu na moja ya fedha huku Isaac Mukani alishinda medali mbili za dhahabu, moja ya fedha na mbili za shaba.

Advertisement

Kati ya medali mbili za dhahabu, moja alishinda katika mita 1500 katika staili ya freestyle.  Salman Yasser pia alishinda medali moja ya dhahabu, tatu za fedha na moja ya shaba.

Muasisi na kocha mkuu wa klabu hiyo, Rahim Alidina aliwapongeza wachezaji wake kwa mataokeo hayo mazuri na kuonyesha jinsi gani klabu inakuwa katika mchezo huo.

Advertisement