Bilionea wa Mlandege anawaza makubwa

Muktasari:

Timu ya Mlandege si kwa ajili ya kufanya biashara ya soka bali ni mapenzi ya bosi wa klabu hiyo kwa ajili ya kusaidia vijana. Kiongozi huyo aliichezea Mlandege miaka ya 80 ambapo pia ni ya mtaani kwao alikokulia Mlandege.

MFAYANYABIASHARA na mmoja wa matajiri wakubwa visiwani Unguja anayemiliki Mlandege FC, Abdul Satar Haji amesema hapati faida yoyote kuwekeza kwenye timu hiyo bali lengo lake ni kurudisha soka la visiwani  kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Satar aliyeinunua timu hiyo miaka mitatu iliyopita aliliambia Mwanaspoti alichukua uamuzi huo baada ya kuona visiwa hivi vina vipaji vingi vya vijana lakini hakuna mtu anayejitolea kuvikuza.
Alisema kununua timu hiyo sio kwamba anataka kufanya biashara ya soka bali ni mapenzi yake kusaidia vijana hasa timu hiyo aliyoichezea miaka ya 80 ambapo pia ni ya mtaani kwao alikokulia Mlandege.
"Nina mipango mingi na hii timu kama uwezo utaruhusu kujenga jengo la klabu pamoja na uwanja wetu,  hakuna faida ninayopata ingawa nafanya kila kitu kuanzia mishahara, usajili na mambo mengine.
"Nafanya hivi kwa kurudisha shukrani kwani hii timu nimeichezea na ilinikuza kisoka hivyo nimeamua kujitolea kwa mapenzi yangu, wanangu ndio waliamua kuifufua maana ilikufa kabisa niliona wazo lao ni zuri ndio maana nimeweka nguvu kuwasaidia vijana.
"Timu yetu haina tatizo lolote na mchezaji anayetaka kuondoka maana anatafuta maisha ila ikidumu kwenye ligi kama miaka miwili basi tutaanza kusajili hata wachezaji kutoka nje ya Zanzibar na Bara,"  alisema Satar
Mlandege ambayo huu ni msimu wake wa kwanza inashika nafasi ya nne kwenye ligi ikiwa na pointi 34.