Biashara Utd kuwasha mitambo kwa Mwadui

Saturday August 11 2018

 

By Masoud Masasi

Mwanza. Kocha wa Biashara United, Hitimana Thierry  amesema mchezo wa kesho Jumapili dhidi ya Mwadui FC ni kipimo tosha kabla ya kuwavaa Singida United kwenye mchezo wa Ligi Kuu Agosti 22.

Mchezo huo kati ya Biashara United dhidi ya Mwadui utapigwa na kwenye Uwanja wa Masondere Kigango, Wilayani Musoma Vijijini.

 Kocha Thierry alisema mchezo huo unatarajiwa kuwa wa mwisho kwao kabla ya kuelekea mkoani Singida kuwavaa Singida United kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu.

Alisema mchezo huo utakuwa kipimo kizuri kwa kikosi chake kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ambapo amesema mpambano huo anauchukulia kwa umakini mkubwa kwani ndio utakaompa kikosi cha kwanza.

Afisa Habari wa timu hiyo, Shomari Binda aliwataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kushudia timu yao.

“Huu nadhani utakuwa mchezo wa mwisho kwetu hivyo ninawaomba mashabiki kuja kwa wingi kuitazama timu yao kwani baada ya hapo tutaelekea mkoani Singida,” alisema Binda.

 

Advertisement