Best 5 mwisho wa utata ile tuzo ni hapa tu

Tuesday July 23 2019

 

By Fadhili Athumani

TUZO ya Ballon d’Or, ni tuzo kila mchezaji hutamani kuipata. Si rahisi kuipata na ndio maana sio wachezaji wote wenye bahati ya kuipata. Kwa mfano, licha ya ubora wao Xavi Hernandez, Thiery Henry na Zlatan Ibrahimovic waliishia tu kunusa harufu yake.

Kwa kipindi cha miaka 10 tuzo hii imekuwa mali ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, kila mmoja akiibeba mara tano. Luca Modric akashinda ya 2018. Ile ya chipukizi ikaenda kwa Kylian Mbappe na Eda Hegerberg akishinda tuzo ya kwanza ya wanawake.

Wakati tukisubiri kuona ni nani watakaoshinda tuzo ya mwaka huu, tayari majina 30 yanayoonekana kuwa na uwezo wa kuingia orodha ya wachezaji bora watakaopigiwa kura. Hawa hapa ni nyota watano wanaotajwa zaidi huko mitaani.

5. MOHAMED SALAH

Licha ya ukweli kwamba Mmisri huyu hakuanza msimu uliopita wa EPL katika kiwango chake bora, ukweli kwamba katika fainali za fainali za mataifa ya Afrika pia hakufanya vizuri na wengi wanamuwaza Riyad Mahrez zaidi yake.

Hatuwezi kusahau kiwango bora alichoonyesha kwa msimu wa mwaka jana wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo alikuwa na mchango mkubwa sana katika ubingwa wa sita wa Ulaya walioupata Liverpool.

Advertisement

Mohamed Salah anastahili tuzo hii bila ubishi wowote. Alizinduka mwishoni mwa msimu na kufanikiwa kumaliza msimu akiwa mfungaji bora wa EPL, kwa mara ya pili mtawalia, akifungana na mchezaji mwenzake Sadio Mane na Straika wa Arsenal, Pierre Emerick-Aubemayang wote wakiwa na mabao 22 kila mmoja.

Najua mjadala mkubwa utaelekezwa katika kuondolewa kwa Pharaohs mapema kwenye AFCON 2019, lakini ikumbukwe kuwa Mo Salah aliyetajwa katika orodha ya watu 100 wenye ushawishi mkubwa duniani ndiye aliyeipelekea Misri katika fainali hizo.

4. EDEN HAZARD

Staa mpya wa Real Madrid, kiungo wa zamani wa Chelsea, Mbelgiji Eden Hazard alianza msimu wa 2018-19 katika kiwango cha juu, ikiwa ni siku chache baada ya kulisaidia taifa lake kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018.

Eden Hazard, alikuwa mmoja wa wachezaji bora kwenye fainali hizo. Waliomshuhudia akifanya vitu vyake huko Urusi watakiri kuwa alikuwa bora zaidi. Aliporejea Stamford Bridge moto wake haukupoa akaisaidia The Blues kutwaa Europa League. Kama hiyo haitoshi, Hazard ambaye amejiunga na Real Madrid kwa dau la Euro 120 milioni, alikuwa na mchango mkubwa katika kampeni ya Chelsea kwenye EPL ambapo alifunga mabao 16 na kuongoza kwa kutoa asisti 15, wakamaliza wa tatu kwenye msimamo.

3. KYLIAN MBAPPE

Dogo wa Ufaransa, bado anaendelea kuukoleza moto huko kwenye Ligue 1. Kiwango chake kinaendelea kupanda. Ndani ya kikosi cha PSG na Ufaransa, Mbappe ni zaidi ya winga. Huyu ndiye mkombozi wao. Mashambulizi yote ya hatari huanzia miguuni mwake.Katika msimu wake wa tatu kwenye Ligue 1, Mbappe alimaliza akiwa na mabao 33 akishindana na Lionel Messi katika vita ya tuzo ya mfungaji bora wa Ulaya. Mwaka jana alitwaa tuzo ya mchezaji bora na mchezaji bora chipukizi wa Ligue 1.

Kama hiyo haitoshi, wakati Luca Modric na Eda Hegerberg wakishinda Ballon d’Or kwa wanaume na wanawake mtawalia, Mbappe alitangaza ujio wa utawala wake kwa kunyakua tuzo ya mchezaji bora chipukizi (Kopa Trophy). Mwaka huu, itakuwaje? Tusubiri!

2. LIONEL MESSI

Murgentina huyu bila ubishi wala kinyongo ni mchezaji bora kabisa kuwahi kutokea katika sayari hii. Nafasi yake katika meza kuu ya wafalme wa soka ni ile wanayojivunia watu kama mpinzani wake Cristiano, Ronaldinho, Zidane, Ronaldo de Lima, Maradona na Pele. Yeye pamoja na Cristiano wametawala tuzo kwa miaka 10. Kabla ya Luca Modric kulitwaa mwaka jana, tuzo hii ilikuwa mali yao. Msimu uliopita alikuwa na mchango mkubwa kwa Barcelona akiisaidia kutwaa ubingwa wa La Liga.

Kikwazo kinachosimama kati yake na tuzo yake ya sita ya Ballon d’Or, ni kuwa katika kikosi ambacho hakikupata nafasi ya kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kama kuna kitu kitakachomzuia ni hicho pamoja na majanga ya Argentina kwenye Copa America mwaka huu.

Lakini utamhukumu kwa lipi mchezaji aliyeibuka kinara wa ufungaji wa mabao barani Ulaya msimu uliopita? Messi alifunga mabao 51 katika mashindano yote msimu uliopita kwa Barcelona iliyobanduliwa kwenye nusu fainali ya UEFA na ubingwa wa La Liga.

1. VIRGIL VAN DIJK

Katika orodha hii yote hakuna mchezaji anayeweza kusimama mbele ya umma na kusema alifanya kazi kubwa msimu uliopita zaidi ya Virjil Van Dijk. Beki huyu ambaye ni mchezaji wa EPL msimu wa 2018-19 ana kila sababu ya kutwaa Ballon d’Or!

Ukuta wa Liverpool umekuwa imara sana baada ya Kocha Jurgen Klopp kutoa Euro 84.65 milioni kuipata saini yake kutoka Southampton. Van Dijk hakufanya kazi ya kuzuia mashambulizi tu, lakini pia alifunga mabao manne katika michezo 38 za EPL. Aliisaidia kutwaa kombe la Klabu Bingwa Ulaya na kuibeba Uholanzi hadi fainali za mataifa ya Ulaya ilikotolewa na Ureno. Ballon d’Or 2019 itaenda kwa nani? Muda utaamua!

Advertisement