Beki wa zamani Yanga SC afariki dunia

Muktasari:

  • Beki wa zamani wa Pan African, Yanga SC na timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Lawrence Mwalusako amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 56.

KLABU ya Yanga na wadau mbalimbali wa soka la Tanzania, wamepokea kwa masikitiko  kifo cha mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Lawrence Mwalusako kilichotokea leo asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.
Enzi za uhai wake, Mwalusako  aliwahi kutamba ndani ya kikosi cha Yanga na timu ya taifa  ya Tanzania 'Taifa Stars' na pia mwaka 2012 kushika nafasi ya ukatibu Mkuu ndani ya klabu hiyo aliyowahi kuichezea miaka ya nyuma.
Hassan Bumbuli ambaye ni Ofisa Habari wa Yanga, alisema kifo cha Mwalusako ni pigo kubwa kwao kwa sababu mbali ya kuitumikia klabu hiyo kwa kipindi kirefu alikuwa sehemu ya waliokuwa wakipigania mabadiliko.
"Tulipokea taarifa za kifo chake saa moja asubuhi. Hili ni pigo kwa familia ya michezo nchini na sio kwa Yanga tu. alijitoa kuichezea kwa moyo na hata kuiongoza kama katibu.
Tunaendelea kufanya mawasiliano na familia ili kushirikiana nao," alisema Bumbuli
Nyota wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba 'Tekelo' ambaye alicheza na marehemu katika miaka ya 80, alimuelezea Mwalusako kwa kusema alikuwa zaidi ya kiongozi wakati huo wakivaa pamoja jezi ya Yanga.
"Alijua namna ya kuitumia elimu yake uwanjani, alikuwa msomi. Nakumbuka alikuwa akituongoza kwa kutuelekeza mambo mengi tukiwa uwanjani.
Tumefanya mengi pamoja hata baada ya kustaafu soka. Nakumbuka aliwahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka," alisema Tekelo.
Naye  mchezaji wa zamani wa Simba SC, Zamoyoni Mogella alimuelezea marehemu kwa kusema anakumbuka vile ambavyo walishirikiana pamoja katika majukumu ya timu ya taifa katika miaka ya 80.
"Alikuwa mchezaji mahiri na muungwana sana, lakini kazi ya Mungu haina makosa. Nakumbuka tulifahamiana zaidi tulipokuwa timu ya taifa kipindi hicho kocha akiwa marehemu, Joel Bendera, tuliwahi kusafiri wote mara kadhaa katika michezo mbalimbali ya mashindano.
"Miongoni mwa michezo ambayo tulisafiri wote ni ule wa mwaka 86 kama sikosei ambapo tulicheza dhidi ya Ethiopia, tulicheza vizuri sana na kulikuwa na vituko sana katika huo mchezo, sikumbuki vizuri kama hatukutoka sare basi walitufunga mabao 2-1, kibaya ni kuwa jamaa hawakuja katika marudiano tukapita," alisema Mogella.