Beki Yanga huyooo Azam

Muktasari:

  • Baada ya kuwapo taarifa hizo, Mwinyi aliliambia Mwanaspoti muda ukifika wa kuzungumzia usajili wake, kila kitu kitawekwa wazi na hilo litafanyika mara baada ya kumalizika kwa ligi.


ZIKIWA zimebaki mechi mbili za kumuacha huru, beki wa Yanga, Haji Mwinyi anahusishwa kuwindwa na klabu ya Azam FC kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Mwinyi ambaye hakuwa na msimu mzuri chini ya kocha Mwinyi Zahera akipoteza namba katika kikosi cha kwanza baada ya usajili wa Gadiel Michael, mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu.

Baada ya kuwapo taarifa hizo, Mwinyi aliliambia Mwanaspoti muda ukifika wa kuzungumzia usajili wake, kila kitu kitawekwa wazi na hilo litafanyika mara baada ya kumalizika kwa ligi.

“Mkataba wangu na Yanga unamalizika msimu huu. Baada ya hapo nitakuwa huru. Nakaribisha klabu yeyote inayohitaji huduma yangu kwa msimu ujao waje tukae mezani tuzungumze, lakini kuhusiana na ofa nilizonazo mezani hadi sasa siwezi kuweka wazi hadi hapo nitakapomaliza msimu wangu kwa michezo miwili iliyobaki,”

“Sikuwa na namba kikosi cha kwanza, lakini hiyo haina maana kwamba kiwango changu kimeshuka, nipo vizuri na nina uwezo wa kupambana. Kutokana na uzoefu nilionao na naweza kucheza timu yeyote.”