Beki Spurs ang'ata ulimi ishu Mourinho

Friday January 24 2020

Hotspur, Toby Alderweireld -Beki Spurs ang'ata ulimi  ishu Mourinho- kocha Jose Mourinho.-

 

LONDON, ENGLAND . LISEMWALO lipo wanasema na kama halipo basi linakuja. Beki wa kati wa Tottenham Hotspur, Toby Alderweireld anajaribu kuficha ukweli kwamba wachezaji wa timu hiyo wanamsikilizia kocha Jose Mourinho.
Kumekuwa na ripoti kwamba mastaa wa Spurs hawafurahii mbinu za ufundishaji za kocha Mourinho na kuna wasiwasi mkubwa kwamba jambo hilo linaweza kuibua mtafaruku kwenye vyumba vya kubadilishia.
Iliripotiwa wiki iliyopita kwamba wachezaji wa Spurs wamechoshwa na mbinu za kizamani za Mourinho ambazo amekuwa akizitumia kuwafundisha wababe hao wa London tangu alipochukua mikoba Novemba mwaka jana.
Lakini, Alderweireld, ambaye alisajili mkataba mpya mwezi uliopita, anajaribu kuficha na kusema kwamba mbona kila kitu kipo vizuri licha ya baadaye kukiri kwamba matokeo yamekuwa hovyo ndani ya uwanja, ambapo kwenye mechi tano za mwisho kwenye ligi wameshinda moja tu.
"Kwangu mimi, sioni kama kuna hicho kitu ," alisema.
"Kama ningeona kuna hicho kitu, nisingesaini dili jipya. Mimi naona mambo yote sawa tu. Tulikuwa vizuri kwa miaka minne au mitano iliyopita, lakini kwa sasa tumeshuka. Kwenye ligi tumekaba koo na timu inayoshika nafasi ya tano, hivyo si mbaya sana. Haina haja ya kukasirika. Sijui hizi taarifa zinafikajefikaje huko. Nawaambia tu tuna furaha."
Mapema wiki hii, The Sun liliripoti kwamba kocha Mourinho anaweza asifike mbali huko Spurs baada ya staili yake ya kutumia mipira mirefu mazoezini kuwachosha wachezaji wa timu hiyo, ikidaiwa mastaa wakubwa wanaponda wanafanya mazoezi ya timu za mchangani.

Advertisement