Beki KMC asisitiza ushindi lazima Taifa

BEKI wa KMC, Abdallah Mfuko amesema haikuwa kazi rahisi kwao kuambulia sare ya bila kufungana katika mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho Afrika na kubainisha kuwa nguvu zote wanahamishia uwanja wa nyumbani.
KMC ambao ni msimu wao wa kwanza kushiriki mashindano ya kimataifa walicheza mchezo dhidi ya AS Kigali walitoka sare ya bila kufungana na wanatarajia kurudiana kati ya tarehe 20 hadi 23 mwaka huu, mchezo huo utachezwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mfuko amesema walijiandaa kwaajili ya ushindi lakini ubora wa wapinzani wao ndio kilikuwa kikwazo kwao kutopata matokeo na kuongeza kuwa wanatambua umuhimu wa uwanja wa nyumbani watapambana kuhakikisha wanawatoa wapinzani wao.
"AS Kigali ni timu nzuri ilitupa changamoto lakini na sisi tulijiandaa kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ili tuweze kuvuka hatua inayofuata kikubwa ni kusawazisha makosa kwa muda huu uliobaki ili kujiimnarisha zaidi kabla ya kushuka tena dimbani,"
"Tulipewa mapumziko ya siku mbili, kesho Jumanne tunaanza kujifua zaidi na mwalimu kupata muda wa kusawazisha makosa aliyoyaona kwetu, tunawaheshimu wapinzani wetu hivyo ni muda wa sisi kuongeza ubora tukiwa mbele ya Watanzania na kuwapa furaha," amesema.