Batshuayi amchongea kocha Chelsea

Muktasari:

Mshambuliaji wa Ubelgiji, Michy Batshuayi, ameendelea kuwasuta waliombeza akiwemo kocha wa zamani wa Chelsea, Antonio Conte, aliyemuuza kwa mkopo kwa madai kuwa hana msaada kwenye timu, mchezaji huyo jana aliifungia Ubelgiji mabao yote katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Iceland katika mechi ya Uefa Nations Ligi.

London, England. Mshambuliaji wa Ubelgiji, Michy Batshuayi ni kama amemsuta na kumchongea aliyekuwa kocha wa Chelsea, Anthonia Conte aliyemuuza kwa mkopo kwenda Valencia ya Hispania.

Batshuayi mwenye miaka 25 jana alifunga mabao mawili akiiwezesha Ubelgiji kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Iceland katika mechi ya Uefa Nations Ligi.

Ushindi huo umeifanya Ubelgiji kuhitaji sare au kufungwa bao 1-0 au sio zaidi ya 2-1 katika mechi ya mwisho ya makundi dhidi ya Uswisi itakayochezwa kesho kutwa kujihakikishia tiketi ya kucheza fainali za Ligi hizo zitakazochezwa Juni mwakani.

Conte alimuuza mshambuliaji huyo chipukizi kwa madai kuwa hana msaada kwa Chelsea, lakini Batshuayi, alijitetea akisema mfumo mbaya wa kocha huyo ndiyo unamfanya asing’ae katika kikosi hicho jambo lin aloonekana kuthibitika.

Mshambuliaji huyo aliyetua Chelsea mwaka 2016 alicheza mechi 32 na kufunga mabao saba kabla ya kuuzwa kwa mkopo Januari mwaka huu kwenda Borussia Dortmund ya Ujerumani alikocheza mechi 10 na kufunga mabao saba na Agosti mwaka huu akauzwa kwenda Valencia kwa mkopo ambako ameshacheza mechi 11 na kufunga bao moja.