Batambuze aumia tena Gor Mahia yahaha

Muktasari:

Fedha hizo zilitokana na mchango wa wanafamilia pamoja na wachezaji wenzake. Baada ya kukusanya Sh350,000 zilizohitajika kwa ajili ya upasuaji huo, alisafiri hadi kwao Kampala Uganda alikofanyiwa upasuaji huo na anatarajiwa kuondoka katika Hospitali ya Kousu hapo kesho.

BEKI mwingine wa Gor Mahia, Shafik Batambuze kafanyiwa upasuaji wa goti miezi saba baada ya kuumia akiichezea klabu hiyo na kisha ikamwachanisha apambane na hali yake.

Batambuze aliachanishwa na Gor baada ya kupata jeraha hilo Aprili alipokuwa akiichezea dhidi ya Ulinzi Stars mechi ambayo waliishia kushinda kwa mabao 2-1.

Mlinzi huyo wa kupanda na kushuka alishindwa kumaliza mchuano huo akipigwa sub katika kipindi cha kwanza.

Tangu kipindi hicho Batambuze aliishi kusaka fedha za kumpeleka hospitalini ili kufanyiwa upasuaji wa kuurekebisha.

Fedha hizo zilitokana na mchango wa wanafamilia pamoja na wachezaji wenzake. Baada ya kukusanya Sh350,000 zilizohitajika kwa ajili ya upasuaji huo, alisafiri hadi kwao Kampala Uganda alikofanyiwa upasuaji huo na anatarajiwa kuondoka katika Hospitali ya Kousu hapo kesho.

Licha ya kuachanishwa na uongozi wa klabu hiyo, Batambuze kaahidi mashabiki wa Gor atajitahidi kuheshimu mkataba wake unaomalizika Novemba mwaka ujao halafu baada ya hapo agure kusaka maisha kwingine.

“Madaktari wameniambia nitahitaji miezi mitano kupona kabla ya kurejea uwanjani. Nashukuru hatimaye nimepata nafuu na labda kikubwa ni kuwaambia mashabiki wa Gor nitareejea kwa kushindo sababu nia yangu ni kuitumikia mkataba wangu hadi tamati,” Batambuze akasema.

Mwenyekiti wa Gor, Ambrose Rachier alipohojiwa ni kwa nini klabu haikuhusikia hata kutoa senti moja kumsapoti Batambuze, wimbo ukawa ni ule ule.

“Mimi bwana ni mkweli na wala sipendi uwongo. Siwezi kudanganya hatukuwa na hela za kumsaidia sababu kama ujuavyo hatuna mdhamini tangu Sportpesa ametuacha hivyo tungewezaje kumsaidia ikiwa kama masuala ya uendeshaji wa klabu bado ni tatizo,” kajitetea.

Miezi kadhaa iliyopita Gor pia ilishindwa kumsaidia beki wake Philemon Otieno afanyiwe upasuaji wa goti na alilazimika kuomba msaada wachezaji wenzake waliomchgangia na kumwezesha afanyiwe upasuaji baada ya kuteswa na maumivi kwa miezi minne tangu alipoumia.