Bartomeu afanya umafya Barca

BARCELONA, HISPANIA. MAMBO yanazidi kuhairibika pale katika kikosi cha Barcelona ambapo mtafaruku mkubwa umeibuka kati ya wachezaji na rais Josep Maria Bartomeu ambaye amekuwa kwenye harakati za kutaka kupunguza mishahara ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kwa sababu uchumi wa klabu umeyumba na bajeti imepungua kwa asilimia 25, kwa sababu ya janga la mlipuko wa COVID-19.

Suala hilo limenekana kupingwa na asilimia kubwa ya wachezaji ambapo Makapteni wote walisaini barua za kuthibitisha kukatwa mshahara, lakini sakata limeibuka upya kwa beki kisiki wa miamba hiyo, Gerard Pique ambaye amesaini mkataba mpya katika siku za hivi karibuni licha yakuwa tayari alisaini barua ya kuka kukatwa mshara.

Kitendo cha staa huyo kusaini mkataba mpya kinaonekana kuwa ni usaliti kwa wachezaji wenzake ambao wameonekana kuwa kwenye mgomo juu ya kujadili jambo lolote na uongozi wa Barca ambao umeonekana kupoteza imani na mashabiki wao.

Ripoti zinadai, viongozi wa Barca walikuwa na kikao na wafanyakazi wote kuhusiana na sakata hilo la kuwapunguzia mishahara lakini wachezaji waliripotiwa kutofika, ikiwa ni moja ya ishara ya kutokubaliana na suala hilo.

Inaaminika, kitendo cha Pique kusaini mkataba mpya ambao utamalizika mwaka 2024 ni moja ya mbinu zilizotumiwa na Bartomeu kuwagawanya wachezaji wote kwenye umoja wao waliouunda hapo mwanzo ili iwe rahisi kufanikisha mchakato huo wa kuwakata mishahara, kwani hakuna mchezaji anayeonekana kumuamini mwenzake kwa kile kilichotokea. Kila mtu akiamini miongoni mwao wachezaji wenyewe kwa wenyewe wapo mamluki na wasaliti ambao wanajiangalia wao tu.

Hivi karibuni kulipigwa kura na matokeo yake yakaonesha wadau na mashabiki wengi wa Barca hawana imani na rais wa sasa wakiamaini ameifanya timu hiyo kuwa katika hali mbaya.