Baridi la Iringa lawaponza Alliance

Muktasari:

  • Nahodha wa timu hiyo, Enekia Kasonga ‘Lunyamila’ aliiomba TFF kuwaangalia waamuzi aliodai wanawanyima uhuru wa kuendeleza vipaji vyao “Kuna wakati unaona kabisa timu pinzani inabebwa, binafsi naona sio kitu kizuri kwa ligi yetu inayotakiwa uwezo ndio uonekane zaidi.

ALLIANCE Girls imeanza ovyo raundi ya pili ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, ikipokea kichapo cha mabao 3-0 mbele ya wenyeji wao Panama Queens ya Iringa, mchezo huo ulipigwa kwenye Uwanja wa Samora.

Kocha wa Alliance, Ezekiel Chobanka alifichua kilicho nyuma ya kichapo hicho kilitokana na hali ya hewa ya baridi kali iliyowafanya kipindi cha kwanza wachezaji wake washindwe kuonyesha makali yao.

Alielezea dakika 45 za kipindi cha pili wachezaji wake walizoea kwa haraka mazingira na kucheza kwa kasi zilizowafanya Panama wapaki basi kulinda mabao 3-0 waliyoyapata kipindi cha kwanza.

“Sio tu naumia kupoteza pointi tatu, bali imenistaajabisha namna tulivyofungwa ndani ya kipindi cha kwanza kutokana na hali ya hewa na laiti kama tungefika Iringa mapema basi tungezoea baridi na isingewasumbua wachezaji wangu,” alisema.

Nahodha wa timu hiyo, Enekia Kasonga ‘Lunyamila’ aliiomba TFF kuwaangalia waamuzi aliodai wanawanyima uhuru wa kuendeleza vipaji vyao “Kuna wakati unaona kabisa timu pinzani inabebwa, binafsi naona sio kitu kizuri kwa ligi yetu inayotakiwa uwezo ndio uonekane zaidi.

Tunasahau matokeo haya tunaelekeza nguvu mechi yetu na Mlandizi tutakayocheza Ijumaa (kesho) Uwanja wa Nyamagana,” alisema.