Bares aisubiri Simba kwa hamu

Friday October 02 2020
bares pic

Dar es Salaam. Kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed ‘Bares’, amesema wala hawana hofu na Simba wanayokutana nayo Jumapili.

JKT Tanzania itaikaribisha Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Hadi sasa, Dodoma FC imecheza michezo minne, ikishinda mmoja, ikitoka sare mmoja na kupoteza miwili, wakati wapinzani wao, Simba wakishinda mitatu na sare mmoja.

Safu kali ya ushambuliaji ya Simba iliyofunga mabao 10 wala haimpi hofu Bares, ambaye timu yake imefunga mabao mawili tu kwenye ligi msimu huu huku akisema kuwa ana mabeki imara ambao wana uwezo wa kuifanya kazi yao.

“Tunaendelea na maandalizi kujiandaa na mchezo huo na hatuna hofu kabisa na Simba kwa sababu ni timu ya kawaida licha ya kwamba ina wachezaji wazuri, mechi itakuwa ngumu.

“Sawa, mechi mbili zilizopita walishinda tena kwa mabao mengi, lakini hilo halitufanyi tuwahofie kwani hata sisi tuko imara tuna kikosi kizuri ambacho kina uwezo wa kuchukua pointi tatu siku hiyo,” alisema Mohammed.

Advertisement

Aliongeza: “Muhimu Mungu atusaidie wachezaji wote waamke salama siku hiyo, lakini mechi tunaichukulia kawaida wala haitupi presha, kwani tuko katika uwanja wetu, tutapambana kupata matokeo mazuri.”

 

Advertisement