Barcelona yawaweka sokoni viungo wake Rakitic, Coutinho

Muktasari:

  • Barcelona imepanga kufanya mapinduzi makubwa kwenye kikosi chake kwa kuondoa baadhi ya wachezaji kabla ya kuleta sura mpya.

Barcelona, Hispania. HII inaitwa safishasafisha. Mabingwa wa La Liga, Barcelona wametoa orodha ya masupastaa wake watano ambao watawekwa sokoni kwenye dirisha hili la usajili na yeyote anayewataka aende tu na pesa akajibebee.

Imeripotiwa kwamba mastaa hao watano ni Philippe Coutinho, Samuel Umtiti, Ivan Rakitic, Malcom na Nelson Semedo, ambao watatajwa kwamba watakuwa wa kwanza kupisha watu wapya wa kuingia huko Nou Camp.

Kwa mujibu wa Marca, Barcelona imepanga kufanya mapinduzi makubwa kwenye kikosi chake kwa kuondoa baadhi ya wachezaji kabla ya kuleta sura mpya. Kwenye mpango huo wapo tayari kumwondoa Coutinho ikiwa imepita mwaka mmoja tu tangu walipomsajili kwa pesa nyingi Pauni 142 milioni kutoka Liverpool Januari mwaka jana.

Taarifa hizo zinadai kwamba Coutinho akiondoka mbadala wake anakuja Antoine Griezmann, huku kwenye ile nanfasi ya Umtiti ataletwa Matthijs De Ligt kutoka Ajax, licha ya taarifa za hivi karibuni kudai dili hilo huenda lisikamilike.

Ivan Rakitic ni staa mwingine ambaye anaweza kuonyeshwa mlango wa kutokea huku kukiwa na klabu kibao kama Arsenal, Manchester United na Inter Milan zikihitaji saini yake. Inter ndio wenye nafasi kubwa na huenda wakamnasa kwa Pauni 43 milioni.

Malcom amekosa namba Nou Camp na anayemtaka anaweza kumpata kwa Pauni 45 milioni tu, huku Semedo akiuzwa kwa Pauni 30 milioni.