Barcelona wambania Suarez kutua Madrid

BARCELONA, HISPANIA. Ukisikia kama noma na iwe noma ndo hii sasa. Luis Suarez ametangaza kuvunja mkataba wake na Barcelona na mabosi wake wameridhia mpango huo.

Hata hivyo, wakaweka masharti mazito ambayo yanaweza kumfanya akasalimu amri na kwenda mahali ambako hakuwa amepanga kabisa.

Iko hivi. Suarez na Barcelona wamekubaliana kuachana kwa amani kabisa baada ya mpachika mabao huyo wa Uruaguay, kuelezwa bayana kuwa hayumo kwenye mipango ya Kocha mpya Ronald Koeman.

Tayari, kulikuwa na mpango wa wazi wa Suarez kwenda kuungana na Cristiano Ronaldo kule Juventus huku harakati za kutua Italia ikiwemo kuomba vibali zikifanyika kwa haraka.

Lakini, ghafla Kocha mpya wa Juventus, Andre Pirlo akaelekeza macho yake kwa straika wa Atletico Madrid, Alvaro Morata, ambaye walipata kucheza pamoja kabla ya kunaswa na Chelsea na baadaye kurejea Atletico.

Kutua kwa Morata ambaye muda mfupi ametua Italia kufanyiwa vipimo vya afya, kukamweka Suarez njiapanda na fasta mabosi wa Atletico wakamuibukia na kufikia makubaliano ya kwenda kuziba pengo la Morata.

Hata hivyo, Barcelona ameibuka na kueleza kuwa Suarez ataruhusiwa kuondoka bure, lakini kuna klabu nne ambazo hatatakiwa kwenda kujiunga nazo. Miongoni mwa klabu hizo ni Atletico Madrid, Real Madrid, PSG na Manchester City.

Kwa mujibu wa Onda Cero, imeelezwa kuwa awali Atletico Madrid haikuwa kwenye klabu ambazo hazitakuwa na nafasi kumnasa Suarez bure, lakini kwa sasa wanafikiria kuweka kiwazo hicho.

Hofu kubwa ya Barcelona kuweka vikwazo kwa Suarez kutua kwenye klabu hizo ni kwamba, wanaweza kukutana naye kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ama La Liga kisha akawafunga, jambo ambalo hawataki litokee.

Mbali na Suarez, Atletico Madrid pia wako kwenye harakati za kunasa saini ya Edinson Cavani, ambaye kama akiungana na kucheza pacha Mruguay mwenzake huyo mambo yatakuwa moto kwelikweli.

Kinachosubiriwa kwa sasa ni Barcelona na Suarez kusaini makubaliano ya kuachana na kama kikwazo cha kujiunga na Atletico kitaondolewa basi atatua kwa Diego Simeone ambako atavuna mshahara wa Euro 8.3 milioni.