Barca yamkosa Thiago kisa Klopp

Wednesday October 14 2020
barca pic

LIVERPOOL, ENGLAND. HABARI ndio hiyo. Barcelona imeripotiwa kutaka kupindua meza dakika za mwisho kwenye usajili wa kiungo Thiago Alcantara, lakini wamekwama kwa sababu Jurgen Klopp alikuwa ameshamaliza kila kitu kumshawishi Mhispaniola huyo kutua Liverpool.

Liverpool ilinasa huduma ya Thiago mwezi uliopita baada ya miezi kadhaa ya kumfukuzia huko Bayern Munich.

Na sasa Thiago ni mchezaji mpya huko Anfield alikotua na kusaini mkataba wa miaka minne na tayari ameshajitengenezea mashabiki baada ya kucheza soka la kiwango kwenye mchezo wake wa kwanza dhidi ya Chelsea.

Bado hajacheza mechi nyingine kutokana na kuambukizwa virusi vya corona, ambapo alikosa mechi mbili dhidi ya Arsenal na ile ya kipigo cha mabao 7-2 kutoka kwa Aston Villa.

Kwa mujibu wa Fabrizio Romano, Barca waliibuka dakika za mwisho kunasa saini ya mchezaji huyo, ambaye yenyewe ndiyo ilimuuza kwenda Bayern Munich mwaka 2013.

Lakini, mwandishi huyo Mtaliano alisema Barca ilichelewa kwa sababu kiungo huyo wa Kihispaniola alikuwa ameshafanya uamuzi wa kutua Anfield baada ya kushawishiwa na Klopp katika mazungumzo waliyokuwa wakifanya kupitia video call.

Advertisement

Thiago alifanya alifanya hivyo baada ya kocha Klopp kumshawishi kwamba kwenye kukipiga katika kikosi cha mabingwa wa England ndiko mahali panapomfaa zaidi.

Thiago hakuwa anafahamu hatima yake kwenye kikosi cha Bayern Munich kabla ya kuhama na hakukuwa na uhakika kama angesaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki Allianz Arena.

Liverpool itarejea uwanjani kukipiga na mahasimu wao Everton uwanjani Goodison Park wikiendi hii katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL).

 

Advertisement