Barca wafungua mlango wa Pep

Muktasari:

Lakini, rais wa Barcelona amesema kitu kuhusu kocha huyo, akisema: “Mimi sikuwa nimehusika. Alikuwa Pep mwenyewe aliyeamua kuondoka, lakini milango ya Barcelona siku zote ipo wazi kwa ajili yake kurudi Barca.”

BARCELONA, HISPANIA . RAIS wa Barcelona, Josep Bartomeu ameibuka na kusema kitu kuhusu Kocha Pep Guardiola baada ya kuripotiwa Manchester City wao wameshaanza kujiandaa na maisha bila ya bosi huyo.

Guardiola yupo mwaka wa nne katika mkataba wake huko Man City na rekodi zake zinaonyesha kwamba hajawahi kuinoa timu yoyote kwa miaka mitano au zaidi.

Mkataba wake utafika tamati 2021 na mwanzoni ilielezwa kwamba angesaini dili jipya, lakini sasa kumekuwa na sintofahamu juu ya hatima ya kocha huyo.

Lakini, rais wa Barcelona amesema kitu kuhusu kocha huyo, akisema: “Mimi sikuwa nimehusika. Alikuwa Pep mwenyewe aliyeamua kuondoka, lakini milango ya Barcelona siku zote ipo wazi kwa ajili yake kurudi Barca.”

Guardiola ameshinda mataji mawili ya Ligi Kuu England tangu alipotua Man City, lakini bado hajafanya chochote kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu alipotua kwenye kikosi cha miamba hiyo huko Etihad.

Taarifa zinadai mabosi wa Man City tayari wameanza kuwa na wasiwasi wa kuhusu Guardiola kama ataendelea kubaki kwenye klabu yake baada ya msimu huu kumalizika, lakini suala la Barcelona kumfungulia milango kocha huyo ili arudi Nou Camp linatoa taswira kubwa ya maisha yanayomkabili kocha wa sasa wa Barcalona, Ernesto Valverde.

Guardiola hivi karibuni alisema hana mpango wa kuondoka Inter Milan, lakini familia yake akiwamo mkewe tayari amesharudi Hispania na hilo ndilo linaloibua mashaka zaidi.