Bao la Mahrez gumzo Afcon

Muktasari:

Mahrez aliyecheza kwa kiwango bora mchezo huo, ameipeleka robo fainali Algeria katika michuano hiyo inayoendelea nchini Misri.

Cairo, Misri. Riyad Mahrez amethibitisha ubora wake uwanjani baada ya kufunga bao maridadi lililochangia ushindi wa Algeria dhidi ya Guinea juzi usiku.

Kiungo huyo wa pembeni wa Manchester City, alifunga bao la pili dakika ya 57 na kuchangia ushindi wa mabao 3-0 iliyopata timu hiyo katika mchezo wa hatua ya 16 bora.

Mahrez aliyecheza kwa kiwango bora mchezo huo, ameipeleka robo fainali Algeria katika michuano hiyo inayoendelea nchini Misri.

Kiki ya mshambuliaji huyo ilikwenda moja kwa moja katika pembe ya kona na mpira kujaa wavuni. Kipa wa Guinea Ibrahim Kone, alishindwa kupangua kiki ya mguu wa kushoto ya nahodha. Bao la nyota huyo limetajwa kuwa moja ya mabao bora katika fainali hizo.

Mabao mengine ya Algeria katika mchezo huo yalifungwa na Youcef Belaili dakika ya 24, Adam Ounas dakika ya 82.

Algeria inaweza kuvaana na Mali au Ivory Coast katika mechi ya robo fainali leo.

Algeria ambayo tangu kuanza fainali hizo, imeonyesha kiwango bora ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi ya kutwaa ubingwa mwaka huu baada ya Cameroon kuvuliwa na Nigeria kwa kuchapwa mabao 3-2.