Bandari FC ni noma, yaja kivingine joh!

Thursday June 13 2019

 

By Abdulrahman Sheriff

MOMBASA. BANDARI FC timu ya pekee kutoka Mkoa wa Pwani inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya, imeamua kuanza kujitayarisha mapema kwa ajili ya msimu mpya wa 2019-2020 kwa nia ya kuhakikisha inatimiza malengo yake ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

Kutokana na thibitisho lilotolewa na Ofisa Mteule Mkuu wa Bandari FC, Edward Oduor, wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi wa timu hiyo wanakutana leo Alhamisi katika Uwanja wa Mbaraki Sports Club kuanza matayarisho ya msimu mpya.

“Kocha Mkuu, Bernard Mwalala anataka timu ianze matayarisho mapema kwa ajili ya msimu mpya na hivyo, wachezaji wote pamoja na maofisa wa benchi la ufundi wanatarajia kuwako uwanjani Alhamisi kuanza mazoezi rasmi,” alisema Oduor.

Katika mahojiano hayo, Oduor alisema hadi wakati huu, hakuna mchezaji yeyote anayeondoka kwa timu na akakanusha kama kipa wao, Farouk Shikhalo ambaye yuko Ufaransa na Harambee Stars hana nia yoyote ya kusajiliwa na Yanga.

“Hadi wakati huu, naweza kusema hakuna mchezaji yeyote wetu atakayetoka timuni na hizo habari za Shikhalo ni za uzushi na uvumi zisizokuwa na msingi wowote,” alisema ofisa huyo.

Mbali na kuhakikisha kuwa wachezaji wao wote wako na hakuna atakayeondoka, Oduor alisema wanasubiri kumsikiliza Kocha Mwalala kama atahitaji mchezaji ama wachezaji wowote kuwaongeza katika kikosi chake.

Advertisement

“Juu ya kusajili wanasoka wapya, hiyo ni juu ya mkufunzi wetu, kutuambia ofisi tuishughulikie lakini hadi sasa tungali tunasubiri atufahamishe matakwa yake,” alisema Oduor ambaye pia hakuweza kuthibitisha ni lini timu  hiyo itakwenda Afrika Kusini baada ya kutwaa taji la SportPesa Shield.

Advertisement