Bandari, Kariobangi Sharks zaibeba Kenya

Saturday January 26 2019

 

UKITIZAMA jinsi timu  za soka zinaumia kupata viwanja vizuri vya soka utafahamu uhaba ulivyo janga nchini. Nchi yote kwa sasa ina kiwanja kimoja tu ambacho kinaweza kuandaa mechi za kimataifa na mabingwa Gor Mahia ndio wanatumia.

Nazungumzia uwanja wa kimataifa wa Moi Kasarani ambao umeandaa mechi zote za Kogalo za kombe la klabu bingwa pamoja na za mashirikisho. Hivi sasa wamefuzu awamu ya makundi ya kombe hili la mashirikisho wakirundikwa kundi moja na Zamalek ya Misri, Petro Atletico ya Angola na Hussein Dey ya Algeria.

Hizi mechi zote sita, tatu zitapigwa ugani Kasarani amini usiamini usitake jua kila mara wana mechi Kogalo hulipa Kshs60,000 kutumia uwanja huo.

Uwanya wa Nyayo hulipwa Kshs40,000 lakini kwa sasa umefungwa kwa miaka miwili sasa kitu ambacho wadau wengi wa soka hawajapendezwa nacho. Kwamba serikali ya Jubilee ulituahidi viwanja vitano vya kimataifa kimegeuka kuwa mchezo wa paka na panya kwani Kenya ilikosa kuandaa mechi za mataifa bora barani kwa wachezaji wa ndani (CHAN) mwaka jana.

Viwanja vya Mumias, Ruaraka, Camp Toyoyo, Thika na Chemelil vilifungwa mara ya kwanza kabla ya wakaguzi wa KPL kuruhusu viwanja vya Ruaraka na Chemelil kutumika kuandaa mechi.

Swali ni je, mbona makocha wangali wanalalamikia hali ya viwanja hivi viwili? Inasemakana hongo ilitolewa ili kuruhusu viwanja hivi viwili kitu ambacho hakitasaidia soka letu. Kocha wa Mathare United Francis Kimanzi alikosoa wakaguzi hao kuruhusu uga wa Ruaraka licha ya vijana wake kuwalaza wenyeji Tusker 2-1 na hivi maajuzi kocha wa Chemelil Francis Baraza akalalamikia sakafu hiyo ya Ruaraka baada ya kupoteza 2-1.

Kwa haya yote lawama kwa serikali tukianza na ya kaunti ya Nairobi ambayo imefeli kukarabati uwanja wa City uliyofungwa mwaka 2013.

Huu ulifaidi sana vilabu vingi haswa Gor Mahia walioutumia kama wao wa nyumbani. Gavana Mike Sonko juzi katika mahojiano na runinga ya Citizen alisema ametenga mabilioni kukarabati viwanja vya mtaani hapa jijini Nairobi lakini hali halisi ni kwamba ni uwanja wa Dandora tu ukarabati unaendelea. Itakuaje gavana anazungumzia kitu ambacho hakifanyiki?

Kaunti ya Nairobi itapokea chapaa nyingi za kuendesha bajeti yao mwaka huu iweje wasitumie asilimia nane tu kujenga viwanja vichache vilivyo mtaani ili timu zetu za daraja la chini zipate sakafu safi ya kucheza?

Naye Waziri wa michezo Rashid Echesa juzi akazuru uwanja wa Kipchoge Keino uliyofungwa pia mwaka juzi kurekebishwa ili kuandaa mechi za CHAN lakini kufikia sasa imebaki story tu.

Echesa aliahidi kufungua viwanja vya Nyayo, Kinoru na huu wa Kipchoge mjini Eldoret lakini kwa sasa hamna chochote kimefanyika. Sio kwamba serikali inakosa chapaa bali muda mwingi ni uzembe wa viongozi.

Iwapo serikali haitambui michezo nchi itaendeleaje? Sasa tumefuzu kombe la mataifa bora barani (AFCON), tutachekelewa sana tukifuzu bila ligi yetu kuimarika hapa nyumbani na hili litafanyika tu mwanzo tukiwa na viwanja vizuri.

Hebu cheki majirani Tanzania wana Uwanja wa Taifa, kisha kuna wa Uhuru na ule wa Azam na yote inaweza kuandaa mechi za kimataifa. Kenya kwa sasa ni mmoja tu wa Kasarani. Serikali basi mbona isiwekeze kampuni za nje kufanyia ukarabati viwanja vyetu kwa miezi kumi na minane tu?

Tuseme kampuni ya Uchina ipewe viwanja kadhaa kufanyia marekebisho wakishamaliza wapewe hela zao waondoke ili Wakenya waanze kulinda na kuhakikisha saa zote viwanja vipo katika hali nzuri. Serikali isipochukulia spoti kwa umakini sioni tukipiga hatua michezoni siku zijazo. Tukutane Viwanjani!

Advertisement